Moshi. Miili ya watu watano waliofariki kwa ajali ya Helkopta ya kampuni ya uokoaji ya Kilimedair meneo ya kati ya Kibo na Barafu Camp, Mlima Kilimanjaro, imetambuliwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, ajali hiyo imetokea leo Desemba 24,2025 saa 11:30 jioni wakati Helikopta hiyo ikitoka kuchukua wagonjwa Mlima Kilimanjaro.
Kamanda Maigwa amesema helikopta hiyo ilikua na watu watano ambao ni Costantine Mazonde raia wa Zimbabwe ambaye alikuwa rubani, Jimy Daniel aliyekuwa daktari na Inocent Mbaga ambaye ni muongoza watalii (Guide).
Wengine waliofariki ni Plos David na Plosova Anna ambao wote ni raia wa Jamhuri ya Czech ambapo walikuwa wageni na walipandishwa Mlima Kilimanjaro na kampuni ya utalii ya Mikaya Tours.
“Ndege ya kampuni ya kilimedair inayofanya kazi za uokoaji Mlima kilimanjaro imepata ajali maeneo ya bonde la barafu majira ya saa 11:30 jioni, helikopta ilikua na watu watano na watu wote wamefariki dunia” amesema Kamanda Maigwa.
Taarifa kutoka eneo la tukio ambazo bado hazijathibitishwa zinaeleza kuwa baada ya helikopta hiyo kuanguka ililipuka moto na kusambaratika huku jitihada za uokoaji zikifanyika.
Eneo la Kibo Hut na Barafu Camp ni urefu wa kati ya mita 4,670 na mita 4,700 kutoka usawa wa bahari.