Askofu Shao: Watu wamekaa kimya siyo kwamba wana amani mioyoni

Unguja. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao amesema watu wamekaa kimyaa lakini siyo kwamba wana amani bali mioyoni wana hasira na mwisho wa hasira hizo unaweza usiwe mzuri.

Askofu Shao amesema ni vyema kukawa na amani ili kuwe na mazingira ya kuzungumzia haki ya kweli lakini kukiwa na migongano na kugawanyika miongoni mwa wananchi haiwezi kupatikana amani na haki vya kweli.

Katika ujumbe wake wa Krismasi leo Desemba 25, 2025 Askofu Shao amesema bila amani hata haki inayodaiwa haiwezi kuwa na mazingira mazuri ya kuizungumzia.

“Ndio maana ya siku ya leo Emanuel Mungu anatembea nasi, watu wamekaa kimya lakini sio kwamba wana amani bali mioyoni wana hasira na hizo hasira mwisho wake sio mzuri,” amesema Askofu Shao.

Amesema “Pamoja na kwamba haki ndio inajenga amani ya kweli ni katika kutafuta haki za watu na ili tuweze kutafuta haki na kuwa na mazungumzo ya haki ni lazima kuwe na amani kwanza tukigawana na kutawanyika kila mmoja na upande wake kuanza vita na malumbano hatutakuwa na mazungumzo ambayo yataleta tija.”

Askofu Mkuu wa Kanisa la Zanzibar International Church Center (ZICC) Kariakoo Zanzibar, Dickson Kaganga amehimiza amani, mshikamano na umoja miongoni mwa wananchi wote.

“Amani na umoja vikawe nguzo yetu, sherehe hizi za krismasi zitukubushe upendo kama Mungu alivyoupenda ulimwengu akamtoa mwanawe wa pekee,” amesema

Amesema wapo wanaotumia siku hiyo kufanya anasa na starehe zilizopitiliza jambo ambalo ni kinyume na dhamira na muktadha wa krismasi.

“Natumia fursa hii kutoa wito kwa wakristu na hata ambao sio Wakristo, tunaposherehekea sikukuu hii, tukumbuke muktadha wake, tunapokwenda kwenye ibada tukitoka tusherehekee lakini kwa uchache tena tukiwa pamoja na wenye uhitaji zaidi,” amesema Askofu huyo wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu

“Tusherehekee kwa amani, tukikumbuka kutoa kama yesu kristo alivyojitoa kwa ajili yetu,’ amesema