Dar es Salaam. Wakiwa na nyuso za furaha huku machozi yakiwalenga na wengine wakishindwa kujizuia na kulia kimyakimya, walinyanyua mikono juu ikiwa ni ishara ya kumshukuru muumba wao, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia kesi ya uhaini vijana saba,
Vijana hao ni waliokuwa wanakabiliwa mashtaka mawili ikiwemo kula njama na kutenda kosa la uhaini.
Sio tu, waliinua mikono juu, bali pia walipinga magoti chini na kunyanyua nyuso zao juu wakiashiria kumshukuru Mungu na kisha kutoa neno moja mbele ya Mahakama hiyo kwa kutamka “Tunamshukuru sana mheshimiwa Hakimu” huku wakimalizia kwa kukunja mikono yao na kisha kuiweka kifuani huku nyuso zao wakiziinamisha chini kuashiria kushukuru.
Hali hiyo ilijidhihirisha hata kwa mmoja wa washtakiwa, Baraka Mwita, ambaye yeye anatumia magongo mawili kutembelea, ambapo lilipofika suala la kuishukuru Mahakama, alilaza chini magongo yake naye kuungana na wenzake kwa kuinamisha kichwa chini na kuweka mikono kifuani, huku akiwa amekaa kwenye kiti kwa sababu hakuwezi kupiga magodi.
Vijana hao ni kati ya washtakiwa 95 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhaini, katika kindi la sita kati ya makundi saba ya washtakiwa waliokuwa wanakabiliwa na kesi hizo katika mahakama hiyo.
Hayo yalijiri jana jioni, Desemba 24, 2025 baada ya Mahakama ya Hakimu Kisutu, kuwaachia huru washtakiwa saba wa kesi ya uhaini inayotokana na maandamano ya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuwafutia mashtaka kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 92 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Sura ya 20, Marejeo ya mwaka 2023.
“Washtakiwa kama jinsi ambavyo Jamhuri walivyoleta ombi lao, mahakama hii inawaachia huru isipokuwa kama mna kesi nyingine ndio mnaweza kubaki” alisema Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Hassan Makube na kuwauliza kama wana kesi nyingine.
Washtakiwa hao walijibu kuwa hawana kesi nyingine inayowakabili na ndipo hakimu alipowaeleza kuwa basi anawaachia huru ili wakajumuike na familia zao.
Waliofutiwa kesi ya uhaini na kuachiwa huru na mahakama hiyo ni Jovin Kaaya, Nelson Abisai, maarufu Chuga, Suphian Massawe, Komba Helbert, Rajab Machonjo, Baraka Mwita na Amasha Juma.
Washtakiwa hao ni kati ya 95 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhaini mahakamani hapo, walioshtakiwa katika kundi sita la kesi hizo.
Hata hivyo, kufutiwa kesi kwa vijana hao saba kunafanya jumla ya washtakiwa 90 wameshafutiwa kesi na kubaki watano, ambao wanaendelea na kesi hiyo.
Washtakiwa hao watano bado DPP anaendelea na mashtaka dhidi yao na pia amewaongezea kesi nyingine. Ambapo mshtakiwa Mohamed Madea (28),maarufu Teacher, Fredy Chacha(21), maarufu Chank na Peter Chobe(49), wao wameongezewa kesi nyingine ya kuchoma moto jengo la CCM Kivule, lililopo Kata ya Majohe wilaya ya Ilala, huku mshtakiwa Tumaini Moshi na Gasper Mmari, wakikabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh1.5 bilioni katika Klabu ya The Voice, iliyopo Kinyerezi.
Hakimu Makube amewafutia kesi hiyo washtakiwa hao saba, baada ya Jamhuri kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kuwashtaki washtakiwa hao katika kesi hiyo.
Kwa mara ya kwanza, walipandishwa kizimbani mahakamani hapo Novemba 7, 2025 na kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Katika kesi hiyo uchunguzi wa awali (PI) namba 26540 ya mwaka 2025, washtakiwa wote walisomewa mashtaka mawili ambayo ni kula njama za kutenda uhalifu wa uhaini na shtaka la uhaini.
Wote kwa pamoja katika shtaka la kwanza walidaiwa kuwa kwa nyakati tofauti kati ya Aprili Mosi na Oktoba 29, 2025 walikula njama za kutenda kosa la uhaini.
Katika shtaka la pili, washtakiwa wote walidaiwa kuwa Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, wakiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitengeza nia kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Washtakiwa hao walidaiwa kuwa walitengeneza nia hiyo kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuithibitisha nia hiyo kwa kusababisha hasara kubwa kwa mali za Serikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.
Ilivyokuwa: Jana washtakiwa hao walipelekwa Mahakamani hapo mchana wakitokea gerezani kwa hati ya dharura.
Tofauti na kesi nyingine, ambapo washtakiwa wa ndani kufikishwa mahakamani hapo asubuhi wakitokea gerezani, jana washtakiwa hao walipelekwa mahakamani hapo mchana na jioni walipandishwa kizimbani na kisha kufutiwa mashtaka yao.
Wakili wa Serikali, Titus Aron aliieleza Mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa kutajwa Januari 5, 2026, lakini washtakiwa hao wamepelekwa mahakamani hapo kwa hati ya dharura.
” Mheshimiwa hakimu, tumewasilisha hati ya maombi kwako inayoitwa Nolle Prosequi ( taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka) kwa mujibu wa kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, Marejeo ya mwaka 2023 kwa washtakiwa hawa saba waliopo mbele ya mahakama yako,” alisema wakili Titus na kuongeza kuwa.
“Kwa mujibu wa kifungu hiki DPP hana nia ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa wote, hivyo kutokana na ombi hili, tunaomba mahakama iwafutie mashtaka na iwaachie huru washtakiwa hawa, ” alisema.
Baada ya kupokea taarifa hiyo ya upande wa mashtaka, Hakimu Makube alisema kwa kuzingatia taarifa hiyo ya DPP anatamka rasmi kuwa kesi hiyo imeondolewa dhidi ya washtakiwa saba.
Hata hivyo Hakimu Makube aliwatahadharisha kuwa licha ya kuwaachia kwa sababu ya DPP kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi dhidi yao, bado anaweza kuwakamata na kuwashtaki tena kwa makosa hayo.
“Hata hivyo kwa mujibu wa kifungu ambacho kilichotumika kuwaachilia, kinaweza kutumika tena kuwakamata na kuwarudisha hapa mahakamani iwapo upande wa mashtaka utajiridhisha kuwa na ushahidi.”
Ndugu waishukuru Mahakama
Mmoja wa ndugu wachache waliofika mahakamani hapo jioni baada ya kupata taarifa kuwa kijana wake wameachiwa huru na Mahakama ni baba mzazi wa mshtakiwa Baraka Mwita, Chacha Mwita ambaye aliishukuru Mahakama, ofisi ya DPP na watu wengine.
“Nawashukuru watu wote, haikuwa rahisi lakini wanashukuru wote, mtoto wangu ametoka, Mungu awabariki” alisema Chacha.
Mzee Chacha licha ya kushukuru, aliomba kupiga picha ya kumbukumbu na washtakiwa waliachiwa huru na mwanaye.
Kwa upande wake mshtakiwa Rajabu Machonjo ambaye ni fundi magari, alisema haikuwa rahisi kwa washtakiwa wenye kesi hiyo kuachiwa huru, lakini wanashukuru Mungu.
“Haikuwa rahisi, hatuamini lakini tunashukuru sana Mahakama na DPP kwa kutuondolea kesi hii” alisema
Uamuzi huu wa kuwaachia huru washtakiwa hao umetokana na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo kwa DPP kuangalia uwezekano wa kuwafutia mashtaka wale watakaobainika kuwa waliingia katika maandamano hayo kwa kufuata mkumbo tu.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo wakati alipozindua na kulihutubia Bunge la 13, Novemba 2025
