Na MASHAKA MHANDO, Tanga
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Tanga (Tanga-UWASA), imetangaza neema ya upatikanaji wa maji kwa miaka 20 ijayo kwa wakazi wa miji ya Tanga, Muheza, Mkinga na Pangani, kufuatia utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa Hatifungani ya Kijani (Green Bond).
Mradi huo wa Sh. bilioni 53.12, ambao ni wa kwanza wa aina yake nchini na Afrika Mashariki, unatarajiwa kukamilika Machi 2026 na utakuwa mwarobaini wa kudumu wa changamoto ya usambazaji maji kwa asilimia 100 katika wilaya hizo nne.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa Tanga-UWASA, Mhandisi Salum Ngugi, wakati wa ziara ya waandishi wa habari kutembelea chanzo cha maji cha Mabayani na kituo cha kusukuma maji cha Mowe.
Mhandisi Ngugi alisema mradi huo ni jibu la changamoto iliyodumu tangu mwaka 2010, ambapo miundombinu iliyosanifiwa kwa miaka 20 tangu mwaka 1978 ilikuwa imezidiwa na kasi ya ongezeko la watu.
“Tulitakiwa kufanya maboresho mwaka 2010 lakini tulikabiliwa na changamoto ya fedha. Sasa kupitia mradi huu mkubwa wa Hatifungani, tunatekeleza malengo makuu matatu yatakayobadili sura ya huduma ya maji Tanga,” alisema Mhandisi Ngugi.
Alifafanua kuwa lengo la kwanza ni kutanua kituo cha kusukuma maji cha Mowe ili kiongeze uwezo wa kusukuma maji kutoka lita milioni 42 hadi kufikia lita milioni 60 kwa siku, wakati mahitaji ya sasa kwa wilaya zote nne ni lita milioni 48 kwa siku.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Ngugi alisema mradi huo utatatua kero ya kukatika kwa maji pindi umeme unapokosekana kwa muda mfupi. Alisema wanajenga tenki jipya la lita milioni 35 ambalo litaunganishwa na tenki la zamani la lita milioni 13, na kufanya jumla ya akiba ya maji kuwa lita milioni 48.
“Kwa sasa ikitokea hitilafu ya umeme hata kwa saa tatu tu, mji unakosa maji. Lakini kwa tenki hili jipya, hata umeme ukikatika, tuna uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa zaidi ya saa 15 bila matatizo yoyote,” alisisitiza.
Mradi huo pia unahusisha ukarabati wa mabomba chakavu yaliyowekwa tangu mwaka 1950 kabla ya uhuru, ambapo sasa yataondolewa yale ya chuma (Cast Iron) na kuwekwa ya kisasa ya plastiki (PVC). Pia, mtandao wa maji utapanuliwa kwa kilomita 60 zaidi ili kufikia maeneo mapya ambayo hayakuwa na huduma hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanga-UWASA, Dkt. Ali Fungo, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ya kisera yaliyofanikisha mamlaka hiyo kupata fedha kupitia soko la hisa.
Mradi huo uliyoanza mwaka 2023 unatekelezwa kwa awamu tatu, ambapo hadi sasa umefikia asilimia 45 ya utekelezaji wake na unatarajiwa kuwa mkombozi wa kijani na kiuchumi kwa mkoa wa Tanga.
MWISHO










