Tabora. Mtoto mwenye umri wa miaka mitatu, Samir Adam mkazi wa mtaa wa Kizigo kata ya Ng’ambo manispaa ya Tabora amefariki dunia baada ya kuzama kwenye shimo lililojaa maji, huku wengine watatu wakisombwa na maji kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya saa nne.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 25,2025 baba mzazi wa mtoto huyo amesema wakati amelala akaitwa na mama yake na kumpa taarifa kuwa mwanaye ametumbukia kwenye shimo, na baada ya kutoka akakuta mwanaye ameshazama kwenye maji,hivyo akamuokoa lakini hospitali wakasema ameshafariki.
“Nimerudi nyumbani nimechoka nikaamua kupumzika mda mfupi tu mamaangu aliniita na kuniambia mtoto amezama kwenye shimo,nimejitahidi kumuokoa mwanangu lakini amefariki tayari naumia sana”amesimulia baba mzazi.
Shimo ambalo amezama mtoto Samir Adam na kufariki dunia katika mtaa wa Kizigo manispaa ya Tabora.
Ester John jirani wa mtoto Samir Adam amesimulia kuwa akiwa nyumbani kwake akasikia jirani yake analia kwa sauti na baada ya kuuliza akaambiwa mtoto Samir amezama kwenye maji lakini pia amepelekwa hospitali amefariki.
“Nimeumia sana kwa sababu Samir ni kajukuu ketu hapa tunacheza nako kila wakati ni katoto kazuri,kana nidhamu na kachangamfu sana yaani mimi kama bibi nimepata maumivu mno,”amesema jirani.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kizigo kata ya Ng’ambo, Grayson Samwel amesema ameshaweka mikakati ya kuwachukulia hatua wale wote walioacha mashimo hatarishi kwani tayari angalizo lilishatolewa hapo awali, lakini wengine wamekaidi na kuendelea kusababisha maafa kama vifo vya watoto kwani kifo cha Samir sio cha kwanza kutokea eneo hilo.
Bodaboda akisaidiwa kuvuka baada ya kuzidiwa na maji kata ya Mwinyi manispaa ya Tabora.
“Hapa tumeshakaa vikao kabisa tukapeana maelekezo juu ya maeneo yote hatarishi kila mmoja achukue tahadhari kwenye eneo lake na hili sitalifumbia macho,kwa sababu mashimo kama haya yanagharimu maisha ya watu akiwemo mtoto huyu leo amepoteza maisha kwa shimo la mtu kaacha hapa”amesema mwenyekiti
Katika matukio mengine katika kata ya Malolo na Mwinyi watu watatu akiwemo mtoto mmoja wameokolewa baada ya kusombwa na maji ya mvua wakati wakivuka barabara maeneo ya Mwinyi na mtaa wa Kombomasai kata ya Malolo.
Waliosombwa na maji ni mwanamke mmoja, boda boda pamoja na pikipiki yake pamoja na mtoto mmoja aliyekua akivuka barabara, ambapo Jeshi la imamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo hayo wamewaokoa watu hao.
Aidha Kamanda wa zimamoto Mkoa wa Tabora, Loshipay Laizer amebainisha kuwa jeshi hilo linaendelea na doria kuhakikisha wananchi wote wanaopata changamoto wanaokolewa kwa haraka, huku akiendelea kutoa wito kwa wananchi kutoacha mashimo wazi kwani ni kinyume pia cha sheria.
“Sisi tunahakikisha tunawaokoa wananchi wetu wanaopata changamoto na pia watupe taarifa za matukio katika maeneo yao,”amesema
