RC Mhita asherehekea Krismasi na watoto wenye uhitaji

Shinyanga. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita amewataka ndugu wa watoto wenye uhitaji kujiongeza pale wanapoona watoto hao wanapungukiwa kwa sababu kuna baadhi yao wanatelekezwa na wazazi na kuishi katika mazingira magumu.

Akizungumza leo Desemba 25, 2025 katika hafla fupi ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi na watoto hao Mhita amesema kuwa, viongozi wanatakiwa kuziba sehemu ambayo inapengo kwa watoto hao,

“Leo wakati kila mmoja wetu yuko na wanae pamoja na wapendwa wake, na sisi tumeamua kujiongeza kwa hawa watoto kujumuika kwa pamoja na kusherekea siku hii na kuleta tabasamu kwao,” amesema Mhita.

Pia ameongeza kuwa, “Sikatai kuwa muda familia zinatengana kwa sababu fulani lakini baba zetu muwe na tabia ya kuonyesha ile nafasi ya baba kwa watoto hata mkitengana, baadhi yenu mkigeuka, mmegeuka hamrudi” ameongeza Mhita.

Aidha, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi amesisitiza kuwa, “Kila mmoja katika jamii awe mlinzi wa mtoto wa mwenzie katika kuwalinda na vitendo vya ukatili tupaze sauti mapema ili wasaidiwe haraka,” amesema Magomi.