::::::
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa zawadi ya vitu mbalimbali kwa vituo viwili vya watoto yatima jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya shukrani kwa walipakodi ambayo hufanyika mwezi wa kumi na mbili kwa kila mwaka.
Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda akikabidhi zawadi hizo amesema wamekuwa na utaratibu wa kurudisha kwa jamii zenye uhitaji kiasi kinachokusanywa kama sehemu ya shukrani na kuonyesha umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari.
“Kwetu sisi mwezi wa 12 ni mwezi wa Shukrani na tumekuja kuwatembelea watoto ikiwa ni sehemu ya shukrani badala ya kuwashukuru kwa maneno tumeamua kuja kutoa hizi zawadi, asanteni sana” amesema Mwenda.
Amesema kutolewa kwa zawadi hizo ni kuomba walipakodi waendelee kulipa kodi kwa hiari na kuchangia maendeleo ya nchi.
Mchango wa Serikali kwa vituo hivyo unatokana na kodi ambazo zimekuwa zikikusanywa na TRA hivyo kila mmoja anapaswa kuwa balozi wa kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari ili kuwezesha kufikiwa kwa wahitaji wengi Zaidi.
Hilda Mtalemwa na Winifrida Malumbo ni wasimamizi wa vituo hivyo ambao kwa nyakati tofauti wameishukuru TRA kwa kutoa zawadi hizo za Krismas ambazo zimegusa maisha ya watoto wanaolelewa katika viyuo wanavyoviongoza.
Wamesema watakuwa mabalozi wa kuhamisha ulipaji wa kodi kwa hiari wakishirikiana na watoto wanaowalea ambao ndiyo walipakodi wa kesho.
Elia Gondwe ni miongoni mwa wazazi wa watoto wanaohudumiwa na kituo cha Uyakonia ambaye amesema ulipaji wa kodi kwa hiari ndiyo umewezesha TRA kutoa misaada kwa watoto wenye uhitaji maalum na kuwaomba wananchi kuwa waaminifu katika ulipaji wa Kodi.
Vituo vilivyokabidhiwa misaada hiyo ni kituo cha Hisani Orphanage Centre na Kituo cha Uyakonia kinachosimamiwa na Kanisa la Kiinjili la Kiluther Dayosisi ya Mashariki na Pwani kwa kushirikiana na Serikali.
= = = = = = =








