Wanne wafariki kwa kuangukiwa na ukuta kanisani, 12 walazwa Dodoma

Dodoma. Watu wanne wamepoteza maisha na wengine 17 kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa Kanisa.

Tukio hilo limetokea jioni ya Jumatano Desemba 23, 2025 katika Kijiji cha Wiliko, Kata ya Mlowa Wilaya ya Chamwino ambapo ukuta wa Kanisa Reality Of Christ Dodoma (ROC) ulianguka wakati waumini wakiwa ndani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa Dodoma, Gallus Hyera hakupatikana kuzungumzia tukio hilo kwani mara kadhaa simu yake ilipopigiwa haikuwa hewani.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Wiliko, Gabriel Mika amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kueleza sababu kwamba ilitokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali.

“Ni kweli amefariki mwanaume mmoja na wanawake watatu wote ni watu wazima wa kijijini kwangu, hapa nipo msibani, amesema Mika.

Amesema siku ya Jumatano mchana kulikuwa na ibada ya ubatizo na ushirika ambapo waumini wengi walikusanyika kanisani hapo na wakati ibada ilipofika mwisho, ilishuka mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali.

“Mchungaji aliwaomba waumini kurudi majumbani lakini wengi wakaona heri wajifiche hapo ndipo ukaanguka ukuta wa jengo hilo, eneo la tukio tulimpoteza watu wawili na hawa wawili walifia hospitali kabla ya kupata matibabu,” amesema Mika.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti, majeruhi walikuwa 17 ambapo baada ya wawili kupoteza maisha, walibaki watano wanaoendelea kutibiwa hospitali ya rufaa ya Dodoma.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ernest Ibenzi amekiri kupokea majeruhi 12 wa tukio hilo ambao amesema wanaendelea na matibabu.

“Sisi tulipokea majeruhi 12 kutoka katika tukio hilo, tunashukuru Mungu kwamba wote wanaendelea vizuri na matibabu hapa hospitali na hatuna kingine tofauti tangu walipoletwa hapa,” amesema Ibenzi.

Katika taarifa aliyotuma kwenye mitandao ya kijamii, Mchungaji wa Kanisa la Reality Of Christ Paul Godfrey, anaeleza jinsi walivyopokea kwa mshituko tukio hilo lakini akaomba waumini wake kujiimarisha katika imani kwani hawana sehemu nyingine zaidi ya hapo.

Mchungaji Godfrey anasema wataendelea kuabudu katika eneo hilo licha ya kuwa hawana jengo la kuabudia lakini eneo hilo ndilo Mungu amewapatia hivyo hawawezi kutoka.