Dube, Diarra mzigoni leo AFCON 2025

RAUNDI ya pili ya mechi za makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 inaendelea leo Ijumaa kwa mechi nne zinazojumuisha timu za Kundi A na B ambazo zina baadhi ya wachezaji wanaotamba katika Ligi Kuu Bara akiwamo kipa Diarra Djigui na Prince Dube wote wa Yanga.

Mapema saa 9:30 alasiri, Angola ilipoteza mbele ya majirani zao za Afrika Kusini kwa mabao 2-1 itajiuliza mbele ya Zimbabwe ya Prince Dube iliyopoteza pia kwa mabao 2-1 mikononi mwa Misri, ikiwa ni mechi inayozikutanisha tena timu za ukanda mmoja wa Cosafa na zinazojuana haswa.

Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Marrakech, huku ikitabiriwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na rekodi baina ya timu hizo, kwani mara ya mwisho kukutana katika makundi ya kuwania kufuzu fainali za Afcon 2013, kila moja ilishinda nyumbani, Zimbabwe ilianza kushinda 3-1 kabla ya Angola kujibu mapigo na ushindi wa 2-0. Katika mechi iliyopita Dube ndiye aliyeifungia Zimbabwe bao kabla ya Misri kuchomoa na kuibuka na ushindi wa dakika za lala salama na leo anatarajiwa kuendelea kutegemewa katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo mbele ya Angola.

Baada ya hapo saa 12:00 jioni itakuwa zamu ya Misri dhidi ya Afrika Kusini zote zikiwa na kumbukumbu ya ushindi katika mechi za raundi ya kwanza za Kundi B. Mechi hiyo imepangwa kupigwa kwenye Uwanja wa Adrar uliopo mjini Agadir na itachezeshwa na mwamuzi Pacifique Ndabihawenimana kutoka Burundi.

Mara baada ya mechi hiyo ya Kundi B, saa 2:30 usiku itakuwa ni zamu ya Zambia iliyolazimisha sare ya 1-1 mbele ya Mali itakayoikaribisha Comoros iliyolala kwa wenyeji Morocco kwa mabao 2-0, mechi ikipigwa kwenye Uwanja wa Mohammed V, jijini Casablanca kabla ya Morocco kufunga hesabu za Kundi A saa 5:00 usiku dhidi ya Mali ya Diarra kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, jijini Rabat. Katika mechi iliyopita Diarra anayeidakia Mali na tegemeo la Yanga alikuwa langoni katika sare ya 1-1 dhidi ya Zambia ambayo pia ina nyota wa zamani aliyewahi kuitumikia Yanga, Kennedy Musonda.

Mechi hizo nne ndizo zinatarajiwa kutoa picha halisi ya timu zipi kutoka makundi hayo mawili ya juu kujiweka pazuri kufuzu 16-Bora.

Mshindi yeyote wa mechi kati ya Mafarao wa Misri na Bafana Bafana ya Afrika Kusini atafikisha pointi sita na kujihakikisha moja ya nafasi kati ya mbili za kundi za kwenda hatua inayofuata na iwapo zitatoka sare pia hazitakuwa mbaya kwao kwani zote zitafikisha pointi nne na kukaa kileleni, bila kujali matokeo ya mechi ya mapema kati ya Zimbabwe na Angola zinazosaka pointi zao za kwanza.

Pia hata kwa mechi za Kundi A kama wenyeji Morocco ataondoka na ushindi mbele ya Mali itakuwa imejiwepa pazuri, lakini ikipoteza italazimika kusikilizia matokeo ya mechi ya mapema kati ya Zambia na Comoro kisha kupiga hesabu kwa mechi ya raundi ya tatu wiki ijayo ili kujua inatoboaje kundini.

Ushindi kwa Mali utaifanya ifikie pointi nne na kuongoza kundi, huku matokeo ya Zambia na Comoros nayo yakiwa upande wa Chipolopolo yatawafanya wafikie pia pointi nne na kusubiri mechi za wiki ijayo ili kujua inapenya au kusikilizia kapu la mshindwa bora kwenda 16 Bora ya michuano hiyo.

Hadi kumalizika kwa raundi ya kwanza zimechezwa jumla ya mechi 12 na kufungwa mabao 29 ikiwa ni wastani wa mabao 2.42 kwa kila mechi, huku nyota watatu Elias Achouri wa Tunisia, Nicolas Jackson wa Senegal na Riyad Mahrez wa Algeria wakiongoza orodha kila mmoja akifunga mawili.

Wachezaji hao pia ni kati ya 12 waliotwaa tuzo ya Nyota wa Mchezo kupitia mechi hizo zilizochezwa katika fainali hizo za 35, wakiwa sambamba na wakali wengine akiwamo Brahim Diaz wa Morocco, Lassine Sinayoko wa Senegal, Lyle Fopster wa Afrika Kusini, Omar Marmoush wa Misri, Theo Bongonda (DR Congo), Semi Ajayi (Nigeria), Edmond Tapsoba (Burkina Faso), Amad Diallo (Ivory Coast) na Bryan Mbeumo wa Cameroon aliyeasisti bao pekee na la ushindi la timu hiyo dhidi ya Benin usiku wa kuamkia jana kwenye Uwanja wa Le Grand Agadir.