Unguja. Hospitali ya Wilaya ya Jitimai, Mkoa wa Mjini Magharibi, yenye vitanda 16 vya wajawazito, inapokea zaidi ya wajawazito 30 kila siku, hali inayolazimu kitanda kimoja kulala zaidi ya wanawake wawili.
Kwa mujibu wa hospitali hiyo, idadi ya wajawazito hubadilika kulingana na msimu, ambapo kila mwezi inapokea zaidi ya wajawazito 700. Katika mkesha wa Krismasi, watoto 20 walizaliwa, wakiwemo wake 12 na waume nane.
Hayo yameelezwa leo, Desemba 26, 2025, na Ofisa Muuguzi wa Hospitali ya Jitimai katika Kitengo cha Uzazi, Reuben Benjamin, wakati wa kupokea vifaa mbalimbali vya uzazi vilivyotolewa na Meya wa Jiji la Zanzibar, Kamal Abdusatar Haji, kwa ajili ya wanawake waliojifungua katika hospitali hiyo.
Benjamin pia amesema kuwa, katika operesheni za upasuaji wa uzazi zinazofanyika hospitalini humo, idadi ya wanawake wanaofanyiwa upasuaji ni kati ya wanne hadi wanane.
“Tunavitanda 16 vya uzazi kati ya hivyo vitanda tisa ni kwa ajili ya waliojifungua na vingine saba ni kwa ajili ya wanaosubiri kujifungua na tuna vitanda vitanda vinne kwa ajili ya kujifungulia,” amesema Benjamin na kuongeza ;
“Kwa hiyo kuna uhitaji mkubwa wa vifaa kwani hospitali inakuwa na wazazi wengi hivyo inakabiliwa na uhaba wa vitanda,” amesema.
Amesema kwa mwezi wanakuwa na wajawazito kati ya 400 hadi 700 na kati ya hao wanaojifungua kwa upasuaji ni 130 kwa mwezi.
Hata hivyo amesema wanajitahidi kupunguza uzazi wa upasuaji isipokuwa kwa mjamzito ambaye anakuwa zimeshafanyika njia zote na kushindikana ndio wanalazikika kufanya upasuaji.
“Sasa ukiangalia wastani wa kina mama wanaolazwa wodini na vitanda, kidogo haiposambamba kwa maana ya kwamba vitanda ni vichache kuliko wajawazito ninaopokea,” amesema ofisa muuguzi huyo.
Hata hivyo, amesema licha ya changamoto mbalimbali ikiwemo za uhaba wa vitanda, uongozi wa hospitali umekuwa ukihakikisha kila mzazi anapata huduma anayostahili na kwa wakati bila kupata usumbufu wowote.
Naye Meya wa Jiji la Zanzibar Kamal Abdulsatar Haji amesema msaada wa vifaa vya uzazi kwa wanawake unalenga kuwapa faraja na kuleta tabasamu baada ya uchungu wanaokutana nao wakati wote wa ujauzito hadi kujifungua.
“Tumetoa pampas, wipes na bahasha ndogo kwa ajili ya mtoto akirudi nyumbani apate angalau pa kuanzia kununuliwa mavazi,” amesema Meya.
Amesema kwa sasa Jiji linajipanga kupata mapato katika vyanzo vyake mbalimbali kuhakikisha wanatekeleza miradi mingi ya maendeleo.
Nao baadhi ya wanawake hao waliojifungua licha ya kushukuru kwa msaada huo walipata wakisema ni muhimu katika kipindi hiki cha uzazi, wameomba kuongezwa idadi ya wodi na vitanda ili kupunguza msongamano wanaokutana nao ndani ya wodi moja.
“Tumeguswa, tunashukuru kwani vifaa hivi vitatusaidia katika kuwaweka sawa watoto wetu na sisi wenyewe,” amesema Agness Wilson mmoja wa wazazi hao.
Naye Diwani wa Mwanakwerewe ilipo hospitali hiyo, Fatma Juma Jabu amesema hospitali hiyo ndio kitovu cha mji wa Zanzibar kwa hiyo inahudumia watu wengi wanaozunguka mji huo kulingana na mazingira iliyopo hivyi inahitaji jicho la pekee katika utoaji wa huduma.
Hata hivyo, amesema uongozi wa hospitali hiyo umekuwa na mikakati imara kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi matakwa ya wagonjwa.
