Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia madereva wanne waliokutwa wakiendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa wakati wa sikukuu ya Krismasi.
Pamoja na madereva hao, polisi pia wamewakamata watuhumiwa wengine wa makosa tofauti, ikiwemo umiliki wa silaha za kienyeji na kujihusisha na biashara haramu ya wanyamapori.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa, Desemba 26, 2025, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kamanda Mkama amesema madereva hao walikamatwa baada ya kubainika wakiendesha vyombo vya moto wakiwa na viwango vya juu vya ulevi, hali inayohatarisha usalama wao pamoja na watumiaji wengine wa barabara.
Amewataja waliokamatwa kwa ulevi ni Alexander Mapunda (45) aliyedaiwa kulewa kwa kiwango cha 667.4 mg/100ml, Theodory John (33) aliyedaiwa kulewa kwa 171.4 mg/100ml, Kibaya Simon (31) aliyedaiwa kulewa kwa 408.9 mg/100ml na Yona Agustino (28) aliyedaiwa kulewa kwa 776.8 mg/100ml.
“Oparesheni ilifanyika jana Desemba 25, 2025 Manispaa ya Morogoro na maeneo mengine ikiwa ni sehemu ya juhudi za Polisi kuhakikisha usalama wa raia na mali zao katika kipindi cha sikukuu unaimarishwa,” amesema Mkama.
Katika matukio mengine, amesema katika Kata ya Katindiuka Wilaya ya Kilombero, mkazi wa Ifakara, Hussein Rashid (40), alikamatwa akiwa na silaha ya kienyeji aina ya gobole, risasi saba kinyume cha sheria na vipande 20 vya nyama ya tohe.
“Silaha nyingine aina ya gobole ilitelekezwa na wahalifu waliokuwa wakifuatiliwa na askari katika eneo la Chamwino Manispaa ya Morogoro na Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu bila ya kuwa na ushirikiano polisi haiwezi kutekeleza majukumu ya kuzuia na kudhibiti wahalifu ili kudumisha amani na usalama wa nchi yetu,” amesema.
