UONGOZI wa Fountain Gate uko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa Pamba Jiji, Saleh Masoud Abdallah ‘Tumbo’, baada ya mchezaji huyo kudaiwa kufikia uamuzi huo wa pande mbili ili akapate changamoto mpya.
Nyota huyo aliyejiunga na Pamba msimu wa 2024-2025, akitokea Klabu ya JKU ya kwao visiwani Zanzibar, inaelezwa ameomba mwenyewe kusitisha mkataba wake, huku Fountain Gate ikiwa mstari wa mbele kuiwania saini yake ili atue dirisha dogo.
Mwanaspoti linatambua Pamba haikuwa tayari kumuachia mchezaji huyo, japo baada ya kuandika barua ya kuvunja mkataba wake uliobakia, uongozi umebariki uamuzi huo hivyo, kutoa nafasi kwa Fountain Gate ambayo tayari inadaiwa imemalizana naye.
“Tulipata taarifa muda mrefu kama anashawishiwa na baadhi ya klabu lakini kwa sababu tulikuwa tuna mkataba naye wa mwaka mmoja hatukuwa na shida, ila baada ya kutueleza mahitaji yake tukaona hatuna haja ya kumzuia,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji (CEO), Peter Juma Lehhet amesema baada ya ripoti ya benchi la ufundi ndipo wataamua atakayebakia au kuondoka katika kikosi hicho, japo kwa sasa bado ni mapema zaidi juu ya hilo.
Tangu nyota huyo ajiunge na Pamba ameifungia mabao mawili ya Ligi Kuu, huku mara ya mwisho kufunga ilikuwa ni ushindi wa timu hiyo wa 3-1, dhidi ya Fountain Gate, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara, Novemba 5, 2024.
