Safari ya ujauzito na maajabu yake

Ujauzito ni safari ya kipekee inayobadilisha mwili wa mwanamke kwa njia za ajabu na za kushangaza. Ndani ya miezi michache tu, mwili huanza kufanya kazi kwa viwango visivyo vya kawaida ili kulea na kulinda kiumbe kinachokua tumboni.
Unaweza kuichukulia kama safari ya kawaida? La hasha! Ni safari ngumu yenye mabadiliko makubwa ya mwili ambayo mama hupitia kipindi chote cha ujauzito.
Mfumo mzima wa mwili hubadilika kutokana na mabadiliko ya homoni na ingawa baadhi ya mabadiliko hayo yanaweza kuhisiwa kuwa ya ajabu au yasiyoeleweka, yote hutokea kwa sababu mwili unajiandaa kuhakikisha maisha mapya yanaanza kwa usalama.
Wakati mwingine mabadiliko haya husababisha usumbufu, lakini mara nyingi ni mabadiliko ya kawaida ambayo humwezesha mwanamke kulisha na kulinda ujauzito na kuandaa mwili wake kwa ajili ya ujio wa mtoto.

Kwa kuelewa mambo haya ya kushangaza na kustaajabisha kuhusu safari hii, makala haya  yanakujuza jinsi ujamzito ulivyo na maajabu yake.
 

Kubadilisha ubongo wa mama na tishu za mtoto

Ujauzito hubadilisha ubongo wa mwanamke na tishu za mtoto katika ukuaji. Wanasayansi wanasema kuwa ujauzito hubadilisha ubongo wa mwanamke kwa kipindi cha hadi miaka miwili, ikijumuisha kupunguza seli fulani ili kumwezesha mama kuhusiana vyema zaidi na mtoto na kujiandaa kwa majukumu yake ya malezi.
Katika uchunguzi uliofanywa na wanasayansi nchini Uingereza mwaka 2016, ambao ripoti yake imenukuliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) mwaka 2021,  wanawake 25 waliokuwa wameshika ujauzito kwa mara ya kwanza walionyesha mabadiliko hayo hudumu kwa hadi miaka miwili baada ya kujifungua.

Vipimo vya sehemu tofauti za ubongo hubadilika, sawa na vile vinavyotokea wakati mtu anapovunja ungo na mabadiliko haya husababisha baadhi ya wanawake kupata tatizo la kusahau au kupoteza kumbukumbu kwa muda.
 

Kubadilishana seli na mtoto aliye tumboni

Mjauzito hubadilishana seli na mtoto aliye tumboni. Seli za mtoto zinaweza kusaidia kutengeneza au kurekebisha baadhi ya sehemu mwilini mwa mama.
Mchakato huu, unaojulikana kama ‘fetal-maternal microchimerism’, humaanisha kuwa chembechembe za mtoto huhamia kwenye mkondo wa damu wa mama na kurudi tena kwa mtoto.
Daktari bingwa wa watoto katika Hospitali ya Dar Group, Gloriamaria Kunambi, anasema: “Chembechembe hizi hukaa katika mwili wa mama kwa miongo kadhaa, zikiacha alama ya kudumu kwenye tishu, mifupa, ubongo na ngozi ya mama. Kila ujauzito unaacha alama zake.
Hata kama mimba haifikii muda kamili au ikiwa imetoka, seli hizi bado huhamia kwenye mkondo wake wa damu.”

Utafiti unaonesha kuwa chembechembe hizi zinaweza kusaidia kurekebisha majeraha, ikiwa moyo wa mama utakuwa umejeruhiwa. Pia seli hizi husaidia kuunda aina mbalimbali za seli zinazoweza kurekebisha moyo.
Hivyo, mtoto husaidia kuimarisha afya ya mama, wakati mama naye humlinda na kumjenga mtoto. Hii ndiyo sababu mara nyingi magonjwa fulani hupotea wakati wa mama akiwa mjauzito.
“Inashangaza jinsi mwili wa mama unavyomlinda mtoto kwa gharama yeyote, na mtoto humlinda na kumjenga tena mama ili mtoto akue kwa usalama na kuishi.

 Fikiria juu ya hamu ya ghafla ya kula aina ya chakula fulani inavyomjia mama. Je, mama alikuwa na upungufu gani wa kutaka kula chakula hicho ilhali mwanzoni hakuwahi kukiwaza? Yote hii ni kwa kuwa chembechembe za seli za mtoto zinamfanya awe na hamu hiyo.”

Ladha, harufu
Ujauzito hubadilisha ladha na hamu ya chakula mama mjamzito mara nyingi hupenda vyakula ambavyo awali hakuvipenda na baadhi ya vyakula huwakera.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Kunambi anasema: “Ni jambo la kawaida kabisa kwa mama mjamzito kuchukia baadhi ya vyakula. Ni miongoni mwa dalili za kawaida katika miezi ya mwanzo ya ujauzito. Zaidi ya asilimia 50–90 ya wajawazito hupata hali hii. Na hili hutokana na mabadiliko ya homoni zinazoongezeka kama hCG (human chorionic gonadotropin) na progesterone ambazo huathiri harufu, ladha na mfumo wa mmeng’enyo.

Hali hii ni mojawapo ya njia asili ya mwili kumlinda mtoto kutokana na vitu hatarishi. Wanawake hupata hamu ghafla ya kula chakula fulani, hali inayowezekana kutokana na chembechembe za mtoto ambazo zinamfanya mama atambue virutubisho au upungufu wa madini mwilini mwake.
“Haya yote yanaweza kufanya mama ahisi kuchukia vyakula fulani, hasa vilivyo na harufu kali kama nyama, mayai, au vyakula vya kukaanga. Hii hutokea zaidi katika trimester (miezi mitatu ya ujauzito) ya kwanza, na hutulia kadri ujauzito unavyoendelea kukua,” anasema.

Sada Saidi mkazi wa Gongo la Mboto ambaye ni mjamzito anasema: “Mimi nilikuwa napenda sana wali na maharagwe, yaani nyumbani kwangu kila siku jioni lazima nipike wali hata kama na mboga nyingine lakini maharagwe hayawezi kukosa. Cha ajabu sasa nilipopata ujauzito yaani nikisikia harufu ya wali ninatapika sana, yaani kwa kifupi siupendi hata kuusikia.”

Figo kufanya kazi kwa kasi

Vilevile ujauzito hufanya figo kufanya kazi kwa kasi mara mbili ya kawaida. Figo za mjamzito husafisha damu kwa ufanisi zaidi, ndiyo maana mama mjamzito hujisikia haja ya kwenda chooni mara kwa mara tofauti na asiye mjamzito.

Kondo
Ujauzito huunda kiungo kipya kiitwacho kondo, ambacho hutoa oksijeni na lishe kwa mtoto na huondoa taka mwilini mwake.
Kwa mujibu wa tovuti ya www.apollohospitals.com, Placenta imeunganishwa na mtoto kupitia kitovu na mara nyingi huondoka baada ya kujifungua. Kiungo hiki ni muhimu sana kwa ukuaji salama wa mtoto.
 

Moyo kufanya kazi kwa kasi

Ujauzito husababisha moyo hufanya kazi zaidi, wakati wa ujauzito, kiwango cha damu mwilini huongezeka hadi asilimia 40–50, na moyo hupiga kwa kasi zaidi ili kusambaza damu ya ziada kwa mama na mtoto.

 Kuzalisha homoni ya Estrojen kwa muda mfupi

Mara nyingi mwishoni mwa ujauzito mwili huzalisha estrogen zaidi kwa siku moja kuliko mwanamke asiye mjamzito anayezalisha kwa mwaka mzima. Estrojen ni homoni muhimu kwa kazi ya jumla ya mfumo wa uzazi wa kike, ujenzi wa afya ya mifupa, hisia, kazi ya moyo na mishipa.

Kuvuta harufu kwa kasi zaidi

Ujauzito huongeza uwezo wa mama kutambua harufu, jambo linalomwezesha kuepuka hatari kwa mtoto. Wanawake wengi hupata hali ya kuwa na uwezo mkali wa kutambua harufu.

Hii huaminika kuwa njia ya asili ya kumsaidia mama kuepuka vitu hatarishi kwa mtoto. Mjamzito anaweza kuvuta harufu kwa kasi zaidi ya ajabu inaweza ikawa mbali au karibu lakini anapofika sehemu tuu anahisi harufu ya kitu fulani anachohisi.

Kutanuka kwa pua na kuziba

Homoni za ujauzito husababisha kuvimba kwa vifuko vya hewa, hivyo kuleta tatizo la pua kuziba bila mafua hali inayoitwa ‘pregnancy rhinitis’.

Kulegea kwa mifupa ya nyonga

Wakati wa ujauzito, mwili huzalisha homoni inayoitwa relaxin ambayo hulegeza mishipa ya nyonga kujiandaa kwa ajili ya kujifungua.

Wataalam wanasema homoni hii hulegeza mishipa ya nyonga ili kumsaidia mama kuandaa mwili wake kwa ajili ya kujifungua.
 

Miguu huvimba na kubadilika saizi na  hii husababishwa na shinikizo la damu ya ziada na utunzaji wa maji mwilini, hivyo kufanya miguu kuongezeka ukubwa. Wakati mwingine hata baada ya kujifungua hali hiyo hudumu.

Kubadili hisia
Mabadiliko ya homoni husababisha mabadiliko ya hisia. Mama hupatwa na furaha, huzuni, hofu au msisimko kwa wakati mmoja.
Ni kawaida mama kulia bila sababu dhahiri kutokana na mabadiliko ya kemikali mwilini mwake.
Mabadiliko yote haya ni sehemu ya mwili kuandaa mazingira salama kwa ukuaji wa mtoto. Ingawa baadhi huweza kusababisha usumbufu kama uchovu, kichefuchefu au maumivu ya mgongo, mara nyingi huisha baada ya kujifungua.
Hivyo mama anashauriwa kufuata lishe bora, ufuatiliaji wa kitabibu na uangalizi mzuri. Wataalamu wa afya ya uzazi wanasema mama anaweza kupitia ujauzito kwa usalama huku mwili wake ukifanya kazi ya kipekee ya kuleta uhai mpya.
Dalili zozote za hatari, kama maumivu makali ya tumbo, kutapika mara kwa mara, damu au uchungu usio wa kawaida zinapopatikana, mama anashauriwa kuonana na daktari mara moja au kufika kituo cha afya kwa usalama wake na wa mtoto.