KIKOSI cha Singida Black Stars kinaondoka leo Ijumaa kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya mechi ya kwanza ya ufunguzi ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mlandege itakayopigwa Jumapili ya Desemba 28, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.
Mechi hiyo itakuwa ya ufunguzi wa mashindano hayo ambapo itapigwa saa 10:15 jioni, ikifuatiwa na ya saa 2:15 usiku, kati ya mabingwa mara nyingi Azam iliyochukua taji hilo mara tano itakayocheza dhidi ya kikosi cha URA kutokea kule Uganda.
Katika kikosi hicho cha Singida, mastaa wapya wataanza kuonekana akiwamo mshambuliaji, Joseph Guede aliyerejea baada ya kumaliza mkataba wake wa mkopo na Al-Wehdat SC ya Jordan, ambaye atatumiwa ili iwe sehemu ya kurejesha kiwango chake.
Guede aliyejiunga na Singida Julai 11, 2024, akitokea Yanga, aliitumikia timu hiyo kwa mkataba wa miezi sita tu, kisha kujiunga na Al-Wehdat ya Jordan kwa mkopo, ingawa kwa sasa amerejea tena kukitumikia kikosi hicho kuanzia Januari 2026.
Nyota wengine ni mabeki wa kati, Abdallah Kheri ‘Sebo’, aliyetokea Pamba aliyokuwa anaichezea kwa mkopo akitokea Azam na Abdulmalik Zakaria aliyevunja mkataba wake wa miezi sita uliokuwa umebakia na kikosi cha maafande wa Mashujaa ya Kigoma.
Beki wa kulia, Abdallah Said Ali ‘Lanso’ aliyemaliza mkataba wake na KMC, ni miongoni pia mwa nyota watakaotumika katika michuano ya Mapinduzi na kikosi hicho cha Singida, ambacho kwa sasa kiko hatua za mwisho za kukamilisha pia usajili wake.
Lanso aliyejiunga na KMC Januari 13, 2024, akitokea Mlandege, mkataba wake na kikosi hicho cha Kinondoni unafikia tamati Januari 2026, ambapo tayari makubaliano ya kujiunga na Singida yamefikiwa na kilichobakia ni mambo madogo ya kukamilisha.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Msaidizi wa Singida, Mkenya David Ouma, alisema michuano ya Mapinduzi wanaichukulia kwa usiriasi mkubwa, kwani ndio sehemu nzuri ya kupata mechi kubwa kutokana na ratiba ngumu iliyo mbele yao baada ya AFCON.
“Sisi tunaenda na wachezaji wetu wote ambao hawako katika timu zao za taifa, lengo ni kuitumia vizuri hii michuano kwa sababu baada ya AFCON kuisha tunarudi kucheza mechi za kimataifa za kiushindani, hivyo lazima tujipange,” alisema Ouma.
Katika michuano hiyo inayoshirikisha timu 10 kwa mwaka 2026, Singida imepangwa kundi A na Mlandege, Azam na URA, huku kundi B likiundwa na Simba, Mwembe Makumbi na Fufuni, wakati kundi C kuna Yanga, KVZ na TRA United (zamani Tabora United).
