Utata waliofariki kwenye ajali Krismasi

Handeni. Utata umeibuka kuhusu idadi ya vifo vya watu waliopoteza maisha katika ajali ya gari wakiwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kusherehekea Krismasi na mwaka mpya.

Ajali hiyo iliyoibua utata wa idadi ya vifo, imesababisha vifo vya ndugu wawili, na wengine watatu akiwemo mama na mwanawe.

Inadaiwa kuwa ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Taula, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga, alfajiri ya Desemba 25, 2025.

Ndugu wa marehemu wawili wamesema idadi ya waliokufa kwenye ajali hiyo ni watu watano, huku kauli ya polisi mkoani Tanga ikisisitiza ni mtu mmoja aliyepoteza maisha.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, waliopoteza maisha tayari wametambuliwa, huku taratibu za kusafirisha miili yao zikiendelea kufanyika.

Kauli iliyotolewa jana Desemba 25 na kuendelea kusisitizwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, ni mtu mmoja tu ndiye aliyefariki dunia kutokana na ajali hiyo.

Katikati ya utata huo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, akizungumza kwa njia ya simu amesema mtu mmoja alifariki papo hapo katika eneo la ajali huku wengine wakifariki njiani wakati wakipelekwa Hospitali.

“Pale kwenye eneo la ajali alifariki mtu mmoja baada ya gari dogo kuingia kwenye fuso na wengine walifariki njiani wakati wakipelekwa hoapitali. Lakini zungumza na RPC yeye atakupa taarifa,” amesema mkuu wa wilaya.

Jana, Desemba 25, 2025 Kamanda Mchunguzi alieleza ni mtu mmoja pekee ndiye aliyefariki dunia kutokana na ajali hiyo, akisisitiza mtu huyo alifariki dunia papo hapo.

Akizungumza na Mwananchi, leo Desemba 26,2025 ndugu wa marehemu, Joel Njau, amesema watu watano wamefariki dunia na wote walikuwa kwenye gari moja.

Amesema hadi sasa miili yote mitano imeshatambuliwa na taratibu za kuisafirisha zinaendelea katika Hospitali ya Magunga Korogwe mkoani Tanga ili kupelekwa Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.

Njau amesema kati ya marehemu hao watano, wawili ni ndugu wa familia ya Njau ambao ni Justin Njau na Herman Njau, huku watatu ni marafiki waliokuwa wakisafiri pamoja kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro.

“Tayari miili yote mitano imetambulika, huyu mwanamke pamoja na mtoto ndiyo walichelewa kutambulika, lakini baada ya kutumia vitambulisho tulivyovikuta kutuma kwenye mitandao ya kijamii, leo asubuhi ndugu zake wamepatikana na sasa ndugu wa marehemu wote wamefika hospitalini na tunakamilisha taratibu za mwisho kabla ya miili kusafirishwa,” amesema.

Baba mdogo wa marehemu Justin, Adam Njau amesema katika ajali hiyo amepoteza ndugu wawili na kwamba kwa sasa wanaendelea na mipango ya taratibu za mazishi.

“Wanafamilia waliopo Tanga wamethibitishiwa miili iliyopo ni mitano na hao wanne ni majirani mmoja anazikwa Uchira mmoja hapa kwetu na mwingine eneo la Kwa Calvin karibu na Kanisa la Katoliki Parokia ya Mnazi hivyo sisi tunajua waliokufa ni watano kwa sababu gari iliyokuwa inatumika ni ya kwetu,” amesema.

Ukiacha taarifa hiyo ya ndugu, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, ameiambia Mwananchi kuwa, katika ajali hiyo, mtu mmoja alifariki dunia papo hapo, huku wengine wakifariki njiani wakati wakipelekwa hospitali.

“Pale kwenye eneo la ajali alifariki mtu mmoja baada ya gari dogo kuingia kwenye fuso na wengine walifariki njiani wakati wakipelekwa Hoapitali. Lakini zungumza na RPC yeye atakupa taarifa,” amesema.

Ameongeza, “mara kadhaa tumekuwa tukitoa onyo na angalizo kwa madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani lakini dereva alikuwa amelewa na hii ni changamoto.”

Katika taarifa yake Mchunguzi, amesema ajali hiyo ilitokea jana 10:30 alfajiri katika Kijiji cha Taula, Wilaya ya Handeni, kwenye barabara kuu ya Chalinze kuelekea Segera.

Alisema ajali hiyo ilihusisha gari dogo aina ya Toyota RunX lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Moshi lililogongana uso kwa uso na gari la mizigo aina ya Mitsubishi Fuso.

Alisema Fuso lilitokea Segera kuelekea Chalinze na Justine Jacobo (32), ambaye alikuwa dereva wa gari dogo alifariki papohapo.

“Uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa Toyota RunX aliyefanya jaribio la kuyapita magari mengine (overtaking) katika eneo lisiloruhusiwa bila kuchukua tahadhari, hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na gari la mizigo,” ilieleza taarifa ya polisi.