MSIMU wa 20 wa michuano ya Kombe la Mapinduzi unatarajiwa kuanza rasmi kesho wakati timu za Kundi A zitakazopokuwa zikikata utepe wa mwaka 2026 katika msako wa taji la michuano hiyo ambalo kwa sasa linashikiliwa na Mlandege ya Zanzibar kwa msimu wa pili mfululizo.
Licha ya kwamba michuano hiyo ilianza zaidi ya miaka 20 iliyopita, lakini rekodi rasmi zinaanzia mwaka 2007 ilipochezwa katika mfumo uliopo sasa hadi leo na katika misimu 18 za awali ilishirikisha klabu mbalimbali za Bara, Zanzibar na za kutoka nje ya nchi.
Mwaka jana pekee michuano hiyo ilishirikisha timu za taifa kutokana na uwepo kwa Fainali za Kombe la Ubingwa wa Afrika (CHAN) 2024 iliyoandaliwa kwa pamoja kati ya Tanzania, Kenya na Uganda na wenyeji Zanzibar ilibeba taji kwa kuwafumua Burkina Faso kwa mabao 2-1.
Katika msimu huu klabu 10 zilipangwa katika makundi matatu zikiwamo Mlandege, Azam FC, Singida Black Stars na URA ya Uganda zimepangwa Kundi A, huku Kundi B lina Simba, Mwembe Makumbi na Fufuni, wakati Yanga, TRA United na KVZ zikipangwa Kundi C.
Michuano ya msimu huu inaanza Jumapili n kufikia tamati Januari 13, ikiwa ni siku moja baada ya maadhimisho ya Miaka 62 ya Siku ya Mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964.
Upo utani Mapinduzi ni michuano ya Azam FC kutokana na rekodi tamu ya kulitwaa mara nyingi taji hilo tangu ilipoanza kushiriki baada ya kupanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2008-2009.
Matajiri hao wa Ligi Kuu Bara, imetwaa taji la Mapinduzi mara tano ikiwa ni rekodi ya michuano hiyo, ikifanya hivyo mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019 katika mechi sita za fainali ilizocheza kwa kipindi chote cha mashindano hayo.
Azam mbali na kuwa kinara wa kutwaa mataji mengi ikiwa ni rekodi, lakini inashika nafasi ya pili kwa kucheza mechi nyingi za fainali ikifanya hivyo mara sita ikilingana na Mtibwa Sugar ambao hata hivyo imetwaa taji hilo mara mbili tu, huku nyingine nne ikizipoteza.
Fainali pekee ambazo Azam ilitinga na kushindwa kutwaa ubingwa ilikuwa ni ya mwaka 2022, ilipolala bao 1-0 mbele ya Simba kwa bao la Meddie Kagere aliyeibuka pia mfungaji bora wa msimu huo.
Azam pia ndiyo timu pekee iliyokuwa ya kwanza kubeba ubingwa wa michuano hiyo na kutetea ikifanya hivyo mara ya kwanza 2012 na 2013 kisha kurudia 2017, 2018 na 2019 na kuandika rekodi mpya ya kuwa timu pekee hadi sasa kuwahi kubeba taji mara tatu mfululizo.
Wekundu wa Msimbazi walipangwa kuanza msimu mpya wa Mapinduzi 2026 dhidi ya Mwembe Makumbi Januari 3 mwakani, ndiyo timu yenye rekodi tamu ya kucheza fainali nyingi zaidi za michuano hiyo ikicheza fainali 10 tangu mwaka 2008.
Hata hivyo, ndiyo timu iliyopoteza mechi nyingi za fainali kuliko timu yoyote kwani Wekundu wa Msimbazi hao wamepoteza sita, huku nne tu ndio wakiibuka na ubingwa wakifanya hivyo mwaka 2008 ilipoifyatua Mtibwa Sugar kwa mabao 2-1, kisha 2011 ilipoikanda Yanga pia kwa mabao 2-1 kisha ikaitambia Mtibwa kwa mara nyingine mwaka 2015 kwa penalti 4-3 baada ya dakika za kawaida kumalizika kwa suluhu na taji la mwisho ililibeba mwaka 2022 kwa kuifunga Azam 1-0.
Hata hivyo, Simba ilichemsha katika fainali nyingine sita zikiwamo tatu mfululizo mbele ya wapinzani, ikiwa ni pekee iliyowahi kuingia fainali nne mfululizo za Mapinduzi ikiwamo ile ya mwaka 2014 ilipofungwa bao 1-0 na KCCA ya Uganda.
Pia ilipocheza fainali za mwaka 2017 kwa kufungwa mabao 2-1 na Azam kabla ya 2020 kulala tena 1-0 mbele ya Mtibwa Sugar na 2021 ikanyooshwa na watani zao, Yanga kwa penalti 4-3 baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu na ndipo 2022 ikajikomboa kwa kuifunga Azam likiwa ndilo taji lao la nne la la mwisho kwani 2024 ililala kwa bao 1-0 mbele ya Mlandege.
Licha ya michuano ya Mapinduzi kufanyikia Zanzibar kila mwaka ni timu mbili tu zilizofanikiwa kubeba ubingwa huo kutokea visiwani, ikiwamo Miembeni iliyokuwa ya kwanza kufanya hivyo katika fainali za mwaka 2009 ilipoizima Mabaharia wa KMKM kwa bao 1-0.
Hata hivyo, kwa misimu miwili mfululizo ya michuano hiyo, Mlandege imefanya balaa kubwa kwa kuipiku rekodi ya Miembeni na klabu nyingine za Zanzibar zilizowahi kucheza fainali za Mapinduzi ikiwamo Jamhuri ya Pemba na Ocean View kwa kubeba ubingwa tena kwa kuvifunga vigogo vya Bara.
Mlandege ilianza mambo 2023 ikiwa chini ya Kocha Abdallah Mohammed Baresi na kubeba ubingwa kwa kuifumua Singida Big Stars kwa mabao 2-1 kabla ya msimu wa 2024 kuinyamazisha Simba kwa bao 1-0 ikiwa ni timu ya kwanza ya Zanzibar kutwaa taji mbele ya timu za Bara.
Kabla ya hapo Ocean View ilikuwa ya kwanza kuicheza na Mtibwa Sugar na kufungwa bao 1-0 mwaka 2010 kabla ya Jamhuri nayo kukumbana na kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Azam mwaka 2012 na baada ya hapo hakukuwa na timu ya visiwani iliyofika fainali hadi Mlandege ilipofanya mambo.
Kwa msimu huu Mlandege inasaka rekodi nyingine mpya iwapo itatetea taji kwa msimu wa tatu mfululizo na kuifikia ile iliyowekwa na Azam iliyofanya hivyo mwaka 2017-2018 na 2019.
Kwa sasa Mlandege inalingana na Mtibwa Sugar kwa kubeba taji hilo mara mbili, licha ya kwamba wapinzani wao walishjapoteza fainali nne kati ya sita ilizoingia tangu 2007, ikianza kupoteza mbele ya Yanga kwa mabao 2-1 mwaka 2007 kisha kurudia tena kwa idadi hiyo 2008 kwa Simba.
Pia ilipoteza mara mbili mfululizo 2015 ilipovaana na Simba na kupoteza kwa penalti 4-3 baada ya dakika za kawaida kumalizika kwa suluhu na 2016 ilifumuliwa mabao 3-1 na URA ya Uganda.
Katika miaka 18 ya michuano hiyo ikishirikisha klabu mbalimbali ni timu mbili za kigeni zote zikitokea Uganda, URA na KCCA ndizo zilizowahi kuondoka na ubingwa wa michuano hiyo, huku Tusker ya Kenya ikichemsha mbele ya Azam mwaka 2013 kwa kufungwa mabao 2-1.
KCCA ndiyo iliyokuwa timu ya kwanza ya kigeni kubeba taji hilo ikifanya hivyo mwaka 2014 kwa kuifunga Simba kwa bao 1-0, kisha URA iliyopo Kundi A na ikitarajiwa kuanza na Azam FC katika msimu huu ikirejea mechi ya fainali ya 2018, ilitwaa taji hilo mwaka 2016 kwa kuifunga Mtibwa Sugar kwa mabao 3-1.
Hata hivyo jaribio la timu hiyo la kutaka kubeba taji kwa mara ya pili mwaka 2018 ilikumbana na aibu mbele ya Azam kwa kufungwa kwa penalti 4-3 baada ya muda wa kawaida kushindwa kufungana, japo ndiyo inayoshikilia rekodi ya kucheza fainali nyingine (mbili) kwa timu za kuitoka nje ya Tanzania.
Safari hii timu hiyo inaanza kazi kwa kukabiliana na Azam kesho Jumapili kabla ya kuja kucheza na watetezi Mlandege kabla ya kumalizana na Singida Black Stars.
Mtibwa Sugar 1-0 Ocean View
Simba 0-0 (p4-3) Mtibwa Sugar
Zanzibar 2-1 Burkina Faso
