KMC yampigia hesabu Nicholas Gyan

KMC inayoburuza mkia Ligi Kuu Bara inadaiwa ipo katika mawindo ya kumnasa winga wa zamani wa Fountain Gate, Mghana Nicholas Gyan kupitia dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa Januari Mosi hadi 31, mwakani.

Timu hiyo ambayo kwa sasa ipo chini ya kocha Abdallah Mohammed ‘Baresi’, ilianza msimu kwa kushinda mechi moja kati ya tisa ilizocheza, huku ikifunga mabao mawili na kufungwa 14 ikishika mkia katika msimamo wa ligi yenye timu 16.

Katika kuhakikisha inarekebisha dosari zilizoifanya kuwa na pointi nne, mabosi wa KMC wameanza kumpigia hesabu Gyan aliyewahi kutamba na Simba misimu kadhaa iliyopita kabla ya kuibukia Fountain Gate.

Gyan hajamaliza msimu na Fountain Gate kutokana na changamoto na sasa ni mchezaji huru akiwa Ghana.

Chanzo cha kuaminika kutoka KMC kimeliambia Mwanaspoti kuwa mazungumzo baina ya uongozi na mchezaji huyo yanaendelea na wanaamini atakuwa chachu ya kuimarisha kikosi kutokana na uzoefu alionao.

“Tayari tumeanza kufanyia kazi ripoti ya benchi la ufundi. Timu yetu haijaanza vizuri msimu ina upungufu mwingi ukizingatia usajili uliofanywa ulikuwa umejaza vijana wengi, hivyo tunahitaji kuongeza nguvu kwa kuzingatia ubora na uzoefu,” kilisema.

“Usajili unafanyika wakati wowote, masuala ya dirisha la usajili ni kukamilisha kile tulichokifanya kwa mazungumzo kwa kukiweka kwenye karatasi na kusubiri uthibitisho. Tumeanza kuzungumza na Gyan, ni winga mzuri anaweza kutupa vitu vingi uwanjani kutokana na kuwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingi.’’

Mwanaspoti lilimtafuta winga huyo ambaye alithibitisha kufuatwa na uongozi wa timu hiyo na kwamba anasubiri simu kufahamu kama watathibitisha kumsainisha mkataba na baadaye kurudi Tanzania. “Ni kweli nimetafutwa na viongozi wa KMC wakinishawishi kujiunga na timu hiyo, nimewaambia nini nakihitaji wakasema watanirudia hivyo simu yao tu,” amesema.