KLABU ya Stand United ‘Chama la Wana’, imefikia makubaliano ya pande mbili ya kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Idd Nassor ‘Cheche’, ikiwa ni baada ya kuiongoza timu hiyo katika mechi 12 msimu huu kwenye Ligi ya Championship.
Kocha huyo wa zamani wa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam, aliliambia Mwanaspoti ni kweli amefikia makubaliano hayo ya kusitisha mkataba wake wa miezi sita uliobaki, kwa lengo la kutoa nafasi kwa mwingine kuendelea pale yeye alipoishia.
“Matarajio ya mashabiki, viongozi na hata wachezaji tangu msimu umeanza yalikuwa makubwa kwangu kutokana na uzoefu wangu mkubwa, ila kwa bahati mbaya nimeondoka kwa sababu kuna mambo ambayo nisingependa kuyaelezea kwa sasa,” amesema Cheche.
Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha pia Pan Africans na Cosmopolitan kwa nyakati tofauti, amesema anaushukuru uongozi wa timu hiyo kwa nafasi waliyompa, licha ya kutofikia malengo ya pamoja waliyoyaweka kutokana na changamoto hizo zilizojitokeza.
Kwa sasa kikosi hicho kinashika nafasi ya 12 kwa pointi 10, baada ya kucheza mechi 12 na kati ya hizo, kimeshinda nne, sare moja na kuchapwa saba, ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao manane na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 16.
