Hutaki mtoto wako awe mnafiki? fanya haya

Dodoma. Fikiria umeitwa shuleni anakosoma mwanao. Kuna tatizo linalowasumbua walimu. Unachoambiwa kumhusu mwanao hakiendani kabisa na kile unachokijua.

“Mnamsingizia mwanangu. Hawezi kuwa hivi mnavyosema,” unabishana nao. Kinachokushangaza zaidi ni kwamba nyumbani mwanao ni mpole na mwadilifu. 

Unajiuliza kimya kimya, “Huu uhalifu ninaoelezwa na walimu umetokea wapi?” Huna majibu, ila unajikuta ukituhumu, “Kwa nini wanamtengenezea mtoto visa?”

Wazazi wengi hupitia hali kama hii. Kile wanachomjua mtoto wao nacho si kile kinachofahamika kwa watu wengine nje ya familia. 

Padri anaweza kumjua mtoto kwa sura tofauti kabisa na ile anayomjua mwalimu. Mwalimu naye ana picha tofauti na ile ya mzazi. 

Mtaani, anapocheza na wenzake, anaonekana kwa namna nyingine kabisa kuliko unyenyekevu anaouonesha nyumbani. Mitandaoni nako, mtoto anaweza kuwa na sura ambayo wale wasiotumia mitandao hawawezi hata kuielewa.

Kuishi kwa kuigiza tabia kunamweka mtoto kwenye hatari nyingi. Kwanza, huanza kupoteza kujiamini. Shinikizo la kuishi kulingana na matarajio ya watu linaweza kuathiri uhuru wake wa kuwa yeye mwenyewe na, polepole, kumgeuza kuwa “msanii” anayejua kucheza na matarajio ya kila anayekutana naye. Anaishi ili aridhishe mazingira, si kwa uhalisia wake.

Pili, hali hii humfanya mtoto akose kuaminika. Watu wanapogundua kuwa ana sura nyingi zinazokinzana, huzuka mkanganyiko wa kimaadili unaoweza kuwafanya wamtilie shaka.

Kwa muda, inaweza kuwa vigumu kwake kuaminiwa, hasa katika mambo nyeti yanayohitaji uaminifu wa dhati.

Zaidi ya hapo, mtoto yuko kwenye hatari ya kupoteza mahusiano ya kweli. Kubadilika-badilika kama kinyonga huwafanya watu washindwe kumtambua yeye halisi ni nani.

Hali hii mara nyingi huzaa upweke mkubwa, hasira isiyoeleweka na migogoro isiyo na msingi na wale wanaompenda kwa dhati.

Kama mzazi, una jukumu la kumsaidia mtoto aache kuvaa nyuso mbalimbali ili kukidhi matarajio ya mazingira. 

Hili linahitaji malezi yanayomjengea amani ya ndani, yakimthibitishia kuwa anaweza kuwa yeye mwenyewe bila shinikizo la kuigiza uhusika usio wake.

Swali muhimu ni hili: unawezaje kumsaidia mtoto asione haja ya kutengeneza sura bandia ili aridhishe watu?

Hatua ya kwanza ni kumkubali mtoto alivyo. Kimaumbile, kila binadamu hutamani kujisikia kuwa anatosha kama alivyo. Huu ndio msingi wa kujiamini. Mpe mtoto nafasi ya kuishi kwa uhuru unaomthibitishia kuwa anakubalika kama alivyo.

Hii haimaanishi kufumbia macho mapungufu yake. La hasha! Unaweza kumrekebisha mtoto kwa upendo bila kumfanya ajisikie kuwa unamkataa kwa sababu si kama unavyotamani awe.

Hatua inayofuata ni kumruhusu kuonesha hisia zake na kuziheshimu bila kumlaumu. 

Mtoto anapolia, anaogopa, anakasirika au anafurahi kupita kiasi, mpe nafasi ya kujisikia anavyohisi bila kumkatiza kwa maneno kama “acha kulia” au “usiogope.”

Unapomfanya mtoto ajisikie kuwa unaelewa hisia zake, unapunguza haja ya yeye kujenga ujasiri bandia au kuficha hisia zake ili akubalike.

Vilevile, ni muhimu mtoto ajue kuwa anapendwa hata anapokosea. Onyesha upendo hata pale anaposhindwa kufikia matarajio yako.

Akivunja kikombe au akisema uongo, unaweza kumweleza kosa lake kwa upole bila kutumia adhabu kali. Kauli kama, “Mwanangu, umekosea, nitakuadhibu, lakini bado ninakupenda,” ingawa ni ngumu, humkomboa mtoto kutoka kwenye woga wa kulazimika kumridhisha mtu ili apate upendo. Hali hii hupunguza tabia ya kudanganya na kuigiza.

Pia, mruhusu mtoto awe mdadisi. Udadisi ni sehemu ya asili ya binadamu. Mpe nafasi ya kuuliza, kuchunguza na kujifunza bila vizingiti vikali.

Jenga mazingira salama ya mazungumzo ya wazi. Mshirikishe katika hoja, mpe nafasi ya kutafuta majibu bila kumkosoa kupita kiasi wala kumlinganisha na wengine.

Kumbuka kwamba hakuna anayejifunza bila kufanya makosa. Mpe mtoto ruhusa ya kukosea.

Kwa kufanya hivyo, unamjengea kujiamini na kumfundisha kutokuona aibu kuwa halisi. Mtoto anapojua kuwa anaweza kukosea na bado akakubalika, hujenga tabia inayoanzia ndani, si tabia inayotokana na woga au shinikizo la nje.

Aidha, mzazi naye ana wajibu wa kuwa kielelezo cha uhalisia. Usijifanye mkamilifu ilhali si hivyo.

Pale inapowezekana, onesha hisia zako halisi mbele ya mtoto. Ukiumia, onesha kuwa umeumia. Unamfundisha kuwa kuonesha udhaifu si udhalilishaji, bali ni sehemu ya ubinadamu.

Ni vyema pia kuepuka kumlinganisha mtoto na wenzake au kumwekea matarajio makubwa yasiyolingana na umri wake. 

Hii humsaidia kupunguza mkanganyiko kati ya sura anayojaribu kuionesha hadharani na nafsi yake ya ndani.

Kadri mtoto anavyokua katika mazingira ya aina hii, sura yake ya hadharani na ile ya faragha huzidi kufanana. Hatimaye, hupata amani ya ndani bila hitaji la kuigiza au kujificha. 

Malezi haya yanahitaji subira na kujitathmini kwa mzazi. Kumbuka, malezi si kumlea mtoto awe nakala yako. Unamlea awe kile Mwenyezi Mungu alikusudia awe. Ukilinda hilo, unalinda nakala ya asili aliyokuja nayo mtoto duniani. Huo ndio uhalisia wa kweli.