Dar es Salaam. Wakati Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, George Simbachawene akiweka wazi dhamira ya Serikali kufanya mageuzi ndani ya Jeshi la Polisi baada ya mwaka mpya, wadau wametaka wigo utanuliwe ili watu wengi washiriki.
Kwa mujibu wa wadau, kuna haja ya kukusanya maoni ili kuongeza tija katika mageuzi, ikiwamo kusaidia hadidu za rejea za yale yaliyowahi kusemwa.
Wameeleza hayo kwa nyakati tofauti walipozungumza na Mwananchi baada ya Simbachawene kuweka wazi mpango wa kufanya mageuzi ndani ya jeshi hilo na kurudisha uhusiano wa karibu uliokuwapo kati yao na jamii.
“Wenzetu wa tume ya haki jinai walitoa mawazo mazuri na Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza tusimamie yale mawazo. Mimi naendelea kuchukua kutoka kule, nataka tukitoka mwaka mpya tukae tuangalie mawazo ya tume nini tunaweza kukifanyia kazi,” alisema Simbachawene Desemba 26, 2025 akiwa wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma.
Alisema moja ya mapendekezo ya tume yalikuwa ni kulifanya Jeshi la Polisi la huduma la jamii ili liweze kulinda raia na mali zao na nguvu itumike pale inapohitajika.
“Sheria ipo wazi inaelekeza mtu akamatwaje, kuna kesi ndogo na kesi kubwa lakini kuna ukamataji wa nguvu inatumika lakini hatima ya nchi ipo mikononi mwa Watanzania,” alisema.
Alisema kupitia maboresho hayo, wanalenga kurejesha mahusiano mazuri kati ya polisi na raia ili polisi akipata shida watu wasishangilie, badala yake wananchi wampe pole na kumuona mwenzao.
“Lazima tufanye mabadiliko makubwa, kwanza ya kimfumo na kiutashi kwa mfano mafunzo yetu ya Jeshi la Polisi lazima tuangalie huenda tunapowafundisha tunawafanya wakapambane na wananchi au wakawalinde,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi Desemba 27, 2025, wakili Dominic Ndunguru, amesema jambo hili ni muhimu kufanyika kipindi hiki, kwani kumekuwapo tafiti mbalimbali zinazoonyesha uhusiano kati ya polisi na jamii uko chini.
Amesema tafiti hizo zinazotolewa na wadau mbalimbali zimekuwa zikionyesha Jeshi la Polisi halikubaliki katika jamii hali iliyochangiwa na kuwapo matukio yanayofanywa na polisi.
“Kuna ripoti zimeshafanyika zikaonyesha kuna maeneo yanatakiwa kuboreshwa ndani ya Jeshi la Polisi. Vilio mbalimbali vinavyotokea watu wanafunguliwa kesi wakati bado uchunguzi haujafanyika, anakamatwa anakaa ndani hadi miaka kesi haijaanza, inatajwa na kurudi. Vitu hivi vinaleta kilio ndani ya polisi,” amesema.
Ili kurudisha uhusiano karibu kati ya jeshi hilo na wananchi, ametaka kufanyika hadidu za rejea ya yale yaliyowahi kusemwa au kuandikwa ili kujua nini kinalalamikiwa.
“Waziri anaweza kuwa na watu wake wa ndani wa kupitia kile kilichowahi kusemwa, lakini ni vyema kupata watu wa nje ya polisi kama watu wa dini, mashirika yasiyokuwa ya serikali,” amesema na kuongeza:
“Hii itasaidia kukusanya maoni yote kila upande, watengeneze mkakati ulioshiba au mpango kazi kwa namna ya kuondokana na hayo mambo, wakipanga kwa namna hiyo itaweza kuwa njia rahisi ya kutatua tatizo hili na inaweza kuwa njia ya kudumu.”
Amesema inaweza kutafutwa namna ya kupoza mambo ndani ya muda mfupi, lakini ni vyema kutafuta utatuzi endelevu unaoweza kudumu kwa miaka mingi.
Alimtaka waziri kurejea matumizi ya polisi jamii ambayo awali ilisaidia kuboresha uhusiano wa jamii na polisi.
“Wakati ule kulikuwa na ushirikiano mkubwa na raia walikuwa wepesi kutoa ushirikiano kwa polisi juu ya utoaji wa taarifa ya matukio yanayotokea. Kwa sasa msisitizo wa polisi jamii haupo, ni vyema pia akawekea mkazo hili ili iweze kujitahidi kurudisha hali iliyokuwapo huko nyuma,” amesema.
Kwa upande wake, wakili John Seka, amesema jeshi limekuwa likilalamikiwa kwa ukatili, hawana huduma nzuri kwenye vituo vya polisi, hivyo ni vyema kufanya maboresho kupitia mapendekezo ya wadau.
Kwa kufanya hivyo amesema itasaidia watu kuona polisi kama sehemu wanayoweza kupata huduma kama ilivyo sehemu nyingine duniani.
“Ni vyema kuwe na chombo kingine chenye uwezo wa kusema utendaji wa polisi ili kuongeza imani kwa wananchi, tofauti na sasa mtu akifanyiwa fujo na polisi anatakiwa kwenda kushtaki polisi, hiyo imekuwa ikifanya kuwa na mchezo wa kulindana kwa sababu hakuna mtu mwingine wa kuwachunguza,” amesema na kuongeza:
“Kama wakifanikiwa kwenda huko itakuwa jambo zuri, lakini polisi kwa sasa akifanya ubaya unaenda wapi? lazima kuwe na taasisi itakayochunguza utendaji wa Jeshi la Polisi.”
Wakili Dk Rugemeleza Nshala, aliyewahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), amesema ili kupata mageuzi ya kweli kunahitajika ushirikiano wa wananchi wote na vyama vyote vya siasa.
“Mabadiliko yanayotakiwa ni makubwa, yanatakiwa kuanza na Katiba ya nchi, huwezi kuanza na matawi wakati shina halijaguswa,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe, amesema hali imefika hapo baada ya polisi kuonekana kufanya vitendo kinyume cha weledi, ikiwamo ukamataji wa watu na kuwatesa jambo ambalo limelishushia hadhi Jeshi la Polisi na kufanya wananchi kukosa imani nalo.
“Kitu cha muhimu ni kulirudisha jeshi kwa jamii na kulifanya kuwa chombo cha huduma zaidi, hilo linawezekana kwa kuangalia mtalaa wao. Namna wanavyotoa mafunzo yao, walifundishwa nini kuhusu uhusiano na raia na tuhakikishe kunakuwa na somo la haki za binadamu, lifundishwe na kueleweka,” amesema.
Massawe ametaka kuwapo chombo huru cha uchunguzi cha matendo ya polisi ili wananchi wawe na imani na jeshi hilo, kwani wanajua wakipata shida wanayo sehemu ya kukimbilia hali itakayolifanya lifanye kazi kwa weledi.
“Hata kwenye Tume ya Jaji Chande tulipeleka haya mapendekezo ili wananchi wanapopata shida wapate sehemu ya kulalamika, hivi sasa kunapokuwa na tatizo juu yake, linalalamikiwa na linajichunguza lenyewe. Kukiwa na chombo wataheshimu na kufanya kazi kwa weledi,” amesema.
Januari 31, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini chini ya Mwenyekiti, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, Makamu mwenyekiti Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue na wajumbe tisa, pamoja na sekretarieti yake.
Lengo la kuundwa kwa tume hiyo ilikuwa kupata ushauri na mapendekezo juu ya namna bora ya kuboresha mfumo na utendaji kazi wa taasisi zinazohusika na haki jinai.
Katika muhtasari wa ripoti ya tume hiyo wa Julai, 2023 yalitolewa mapendekezo mahususi kwa Jeshi la Polisi ikielezwa:
“Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vinavyochafua taswira ya Jeshi la Polisi. Malalamiko hayo dhidi ya Jeshi la Polisi yanahusu kushindwa kuzuia uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi, vitendo vya rushwa, mali za watuhumiwa kupotea vituoni na kuchelewa kufika kwenye maeneo ya matukio.”
Hali hiyo ilielezwa na tume kuwa inasababisha wananchi kupoteza imani kwa Jeshi la Polisi na kutokutoa ushirikiano unaotakiwa.
Tume ilipendekeza Jeshi la Polisi lifanyiwe tathmini ya kina itakayowezesha jeshi hilo kufanyiwa maboresho makubwa na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo.
Vilevile, libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra na kuwa Polisi Tanzania ili kutoa taswira kuwa Jeshi la Polisi ni chombo cha kuwahudumia wananchi.
Pia, kubadilisha mitalaa ya mafunzo na mtazamo wa askari wa Jeshi la Polisi ili kutoka katika dhana ya ujeshi kwenda dhana ya kuhudumia wananchi na Jeshi la Polisi liboreshe mfumo wa ndani wa kushughulikia malalamiko ya wananchi.
Mbali ya hayo, liimarishe huduma za intelijensia ya jinai na polisi jamii na kuanzisha programu za kuisogeza zaidi kwenye jamii.
Kuhusu uwajibikaji na usimamizi huru wa Jeshi la Polisi, tume ilieleza ilipokea malalamiko ya kuwapo matukio mengi ya ukiukwaji wa sheria unaofanywa na watendaji wa taasisi za haki jinai, hususani Jeshi la Polisi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa ukamataji, kutesa watuhumiwa wakati wa kuchukua maelezo ya onyo na kubambikia watu kesi.
Tume ilipendekeza madawati ya malalamiko ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi yaimarishwe kwa kuyapatia watumishi wa kutosha wenye weledi kwenye masuala ya uchunguzi ili waweze kushughulikia malalamiko yanayowasilishwa kwenye taasisi hizo ipasavyo.
Ili kushughulikia nidhamu na maadili ya askari na maofisa, ilipendekezwa kuwa muundo wa Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi, Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji uangaliwe ili kiwe chombo kinachotekeleza majukumu yake kila siku badala ya kutekeleza majukumu yake kwa vikao.
