KOCHA mkuu wa Simba, Steve Barker alitarajiwa kutua nchini jana, lakini huku nyuma kukiwa na taarifa ya kushtukiza kutokana na kuumia kwa kipa Yakoub Suleiman ambaye inadaiwa huenda akamponza kipa namba moja wa timu hiyo aliye majeruhi kwa muda mrefu, Moussa Camara.
Yakoub aliumia wiki iliyopita akiwa katika mazoezi ya timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kabla ya kucheza mechi ya kwanza ya Kundi C ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea Morocco, na kuipa pengo pamoja na klabu anayoichezea ya Simba.
Kabla ya Yakoub kuumia huko Morocco, Simba ilikuwa ikimtegemea kikosini baada ya Camara kuwa nje akifanyiwa upasuaji wa goti, lakini kwa taarifa hizo na kitu kinachofanyika ni wazi haitashangaza kusikia kipa huyo raia wa Guinea akiwekwa kando kumpisha kipa mpya wa kigeni.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinadai ripoti ya kitabibu inayoonyesha kuwa makipa hao wanaweza kuwa nje kwa muda mrefu kiasi cha kukosa baadhi ya mechi za makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hiyo ikiwa Kundi D pamoja na Esperance ya Tunisia, Stade Malien ya Mali na Petro Atletico, kumewashtua mabosi wa Msimbazi.
Yakoub anatakiwa kuwa nje kwa mwezi mmoja na siku 10 wakati Camarra ilielezwa angekuwa nje kwa kati ya wiki nane hadi 10 baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti, hivyo kuwaweka wote katika hatihati ya kukosa mechi za mwezi ujao dhidi ya Esperance zinazotegemewa kuifufua Simba.
Ndio, Simba itaanza ugenini dhidi ya wababe hao wa Tunisia, Januari 23, kabla ya kurudiana Dar es Salaam wiki moja baadaye na timu hiyo inahitaji ushindi kutokana na kupoteza mechi mbili za awali dhidi ya Petro na Stade Malien zilizoifanya ishike mkia wa kundi D bila pointi.
Ili kurejea kile ilichofanya misimu mitatu iliyopita 2022-2023 ilipopoteza mechi mbili za awali, lakini ikajitutumua mechi zilizofuata na kutinga robo fainali, Simba inahitaji ushindi angalau wa mechi moja dhidi ya Esperance na hapo ndipo mabosi Msimbazi wanapopiga hesabu za kuleta kipa wa kigeni.
Kwa sasa Simba imesaliwa na kipa mmoja, Hussein Abel, na tayari imeanza msako wa kipa mwingine mzawa wa kusaidiana naye wakati wasikilizia hali ya Yakoub, huku jina na Yona Amosi wa Pamba Jiji na Constatine Malimi wa Mtibwa Sugar yakitajwa kuanza kufuatiliwa.
Hata hivyo, inadaiwa ndani ya Simba mambo huenda yakageuka baada ya viongozi kukubaliana kwa kauli moja juu ya kusaka kipa mwingine wa kimataifa mwenye uwezo mkubwa wa kuibeba timu kama ilivyokuwa kwa Camara.
Kama Simba itafanikiwa kumnasa kipa huyo wa kigeni basi ni wazi kibarua cha Camara kitafikia mwisho kutokana na kanuni mpya ya usajili y Ligi Kuu, kutoruhusu timu moja kuwa na makipa wawili wa kigeni.
Kanuni za Ligi Kuu zinasema kwa wachezaji wa kigeni zinasema, kila timu itaruhusiwa kuwa na wachezaji 12 wa kigeni, lakini kila timu itaruhusiwa kusajili kipa mmoja tu, tofauti na ilivyokuwa misimu iliyopita iliporuhusu klabu moja kuwa na makipa wa kigeni zaidi na mmoja bila tatizo.
Hatari zaidi ni kwamba, Camara aliyeanza kuidakia timu hiyo tangu msimu uliopita aliongeza mkataba wa mwaka mmoja ambao kwa uko ukingoni ukiwa umesaliwa na muda wa miezi sita na kufanya iwe rahisi kwa mabosi wa Msimbazi kumfyeka iwapo watapata kipa mpya wa kigeni wa viwango.
Lakini kama mipango ya Simba ya kuleta kipa wa kigeni itashindikana na iwapo itataka kusaliwa na Camara hadi mwisho wa msimu wakati akiendelea kujiuguza, itabidi imsajili mzawa anakayeungana na Abel ambaye hata hivyo, tangu asajiliwe kutioka KMC hajawahi kuaminiwa klabuni hapo.
Mwanaspoti linafahamu, Simba iko sokoni kwa sasa kusaka kipa mpya atakayeisaidia katika mechi za hatua ya makundi zitakazoanza mapema Januari, ikitaka kulitupia dirisha dogo la usajili linalofunguliwa Januari 1-31 mwakani, huku majina ya Amosi na Malimi yakianza kutajwa mapema.
Simba imesaliwa na mechi nne za Ligi ya Mabingwa kwani baada ya kuvaana na Esperance mara mbili mfululizo mwishoni mwa Januari mwakani, itaifuata Petro Atletico Februari 6 na kumalizana na Stade Mallien wiki moja baadae na kusikilizia kama itapenya kwenda robo fainali au safari itaishia hapo.
Japo la kuvutia ni kwamba mabadiliko madogo ya kanuni za usajili kwa michuano ya CAF imetoa nafasi kwa klabu kusajili hata mchezaji aliyecheza mechi za kimataifa msimu huu, tofauti na ilivyokuwa zamani ikizuia aliyetumika raundi za awali kuchezea timu mpya katika michuano hiyo tena.
