Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwenendo wa Mvua Kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Imeeleza kuwa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha uharibifu wa miundombinu muhimu, ikiwemo reli, barabara na mifumo ya umeme, hali iliyoathiri shughuli za usafiri wa abiria na shehena katika baadhi ya maeneo.
Katika taarifa iliyotolewa na TMA leo Desemba 28, 2025 imeeleza kuwa mvua hizo zimeathiri reli ya zamani ya MGR baada ya madajara kuharibika katika eneo la Kidete wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, pamoja na eneo la Gulwe wilayani Dodoma. Aidha, kumekuwepo na hitilafu za umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na umeme wa reli ya kisasa ya SGR, hali iliyosababisha usumbufu katika utoaji wa huduma za usafiri.
Pia imeeleza barabara kuu ya Morogoro–Iringa, hususani eneo la Mama Marashi hadi Mikumi, imeripotiwa kukumbwa na maporomoko ya mawe na tope yaliyorundikana barabarani, jambo lililosababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo na kuchelewesha safari.
TMA imetoa ufafanuzi kuhusu hali hiyo kuwa ni sehemu ya vipindi vya mvua kubwa vilivyokuwa vimetolewa tahadhari kuanzia tarehe 26 hadi 29 Desemba 2025. Kwa mujibu wa TMA, mikoa iliyotabiriwa kuathirika ni pamoja na Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Dodoma, Singida, Songea, Morogoro, Lindi, Mtwara, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikiwemo Kisiwa cha Mafia) pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
“Hadi kufikia saa 3:00 asubuhi ya leo, vituo vya hali ya hewa vimerekodi viwango vikubwa vya mvua vilivyozidi milimita 50 ndani ya saa 24 katika maeneo ya Same (milimita 94.5), Morogoro (milimita 58.6) na Tabora (milimita 55.4). Vituo vingine vilivyopata mvua ni Hombolo (milimita 49.5), Kibaha (milimita 43.6), Dodoma (milimita 36.6) na Iringa (milimita 35.6).” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
TMA imeeleza kuwa mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuendelea kuimarika kwa ukanda wa mvua, hali itakayochangia kuendelea kwa vipindi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mara, Simiyu, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Lindi na Mtwara kesho tarehe 29 Desemba 2025.
Kwa upande wake, Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua za haraka kurejesha hali ya kawaida katika miundombinu iliyoharibiwa ili kuhakikisha usalama wa wananchi na kuendelea kwa shughuli za kiuchumi huku wananchi wakitakiwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kutoka TMA na kuzingatia ushauri wa wataalam ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.