Mume wangu nikikosea au akikasirika jambo ananisema mbele ya watoto sifurahii tabia hiyo, nifanye nini ili aache maana ananidhalilisha sana.
Pole kwa unachopitia, si jambo dogo wala la kupuuzwa, unapodharauliwa mbele ya watoto wako.
Kwa hili hata mimi nakuunga mkono hupaswi kulifumbia macho bali kulikemea maana linaondoa utu wako mbele ya watu unaopaswa kuwafunza tabia njema.
Watoto hujifunza zaidi kwa kile wanachokiona kuliko wanachosikia. Hivyo, ni hatari kuacha tabia hii iendelee, kwani inavunja sio tu na heshima yako, bali pia na malezi ya watoto.
Mtoto anayeona wazazi wake wakidharauliana mara kwa mara anaweza kuishi na hisia za kutokuwa na thamani au kudhani kuwa dhulumu ni jambo la kawaida.
Uliposema umechoka ni kama umekata tamaa, usikate tamaa mapema, kwani huyo ni mumeo na kikubwa zaidi ni baba wa watoto wako.
Unasema umeshamweleza umechoka, hapana pengine njia uliyotumia kuzungumza naye haikuwa sahihi sana au ilikuwa na msisitizo mdogo.
Hivyo zungumza naye ana kwa ana, ukimueleza kinaga ubaga jinsi anavyoumiza hisia zako kukusema mbele ya watoto, zingatia usilalamike wala kulia bali sema unavyojisikia. Mwambie kwa uwazi na kwa maneno ya hisia zako kwamba tabia ya kukudharau mbele ya watoto inakuumiza sana, inakudhalilisha, na pia inaweza kuathiri watoto kihisia.
Hii ni fursa ya kumwonyesha kuwa maneno unayomweleza sio tu kusema, bali yanatakiwa kuheshimiwa.
Kwa wanawake wengi wenye hekima, hatua ya kwanza ni mazungumzo tulivu, yenye heshima lakini yenye uthabiti. Mwanaume ambaye ana busara na upendo wa kweli atasikia hisia zako na ataona umuhimu wa kubadilika. Lakini dada, kama mazungumzo haya hayaleti mabadiliko, huwezi kubaki kimya.
Hii ni kwa sababu kubaki kimya au kusita kuchukua hatua kunampa mtu nafasi ya kuendelea na tabia isiyofaa, na wewe una haki ya kulinda heshima yako na ya familia yako.
Baada ya mazungumzo haya ya kina kati yako na mumeo, kama ataendelea na tabia hiyo usisite kutafuta msaada kutoka kwa watu unaowaamini.
Wazazi, ndugu wakubwa, au viongozi wa dini ambao wana hekima na wanajali wanaweza kuwa msaada mkubwa. Wakati mwingine sauti ya mtu wa tatu anayeheshimika inaweza kufungua macho ya yule anayekudhuru kwa njia ambazo maneno yako peke yake hayawezi kufanikisha.
Msaada huu si udhaifu, bali ni njia ya hekima ya kuhakikisha usalama wako kihisia na kiakili.
Kwa upande mwingine kumbuka kuwa hakuna mtu anayepaswa kukudhalilisha au kukufanya ujisikie mdogo. Kujilinda kihisia ni ishara ya nguvu na si dhambi. Kuonyesha kuwa umechoka na huwezi kubeba dhuluma zisizoisha ni ishara ya ujasiri.
Una haki ya kulinda hisia zako na kutoa mipaka. Mara nyingine, hatua ya mwisho inaweza kuwa kuanzisha mipaka thabiti au hata kuamua hatua kali zaidi kama heshima yako inaendelea kudhuriwa.
Hii inaweza kuhusisha kutumia muda mbali naye ili kupunguza athari za kudharauliwa au hata kufikiria ushauri wa kisheria ikiwa ni lazima.
Kumbuka kuwa wewe ni binadamu mwenye thamani kubwa. Heshima yako si kitu kinachoweza kuuzwa au kuachwa kwa urahisi.
Watoto wako wanahitaji kukuona ukiwa imara, unajiheshimu na unajilinda. Hii itawafundisha thamani ya heshima na jinsi ya kushughulikia watu wasiowaheshimu. Chukua hatua kwa utulivu na hekima lakini usikubali udhalilishaji uendelee.
