RC BATILDA, MWANAFA WAKOSHWA NA ‘HALE FESTIVAL’

 📍WAHIMIZA ENZI ZA TX MOSHI WILLIAM KUTUMIKA KUIBUA VIPAJI

NA MASHAKA MHANDO, Korogwe

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amemwagia sifa mwandaaji wa tamasha la ‘Hale Festival’, Dkt. Hassan Abbas, huku akibainisha kuwa jukwaa hilo ni daraja imara la kuibua na kuendeleza vipaji vya muziki na soka mkoani humo.

Akizungumza katika usiku wa kipekee wa kumkumbuka gwiji la muziki wa dansi nchini, marehemu TX Moshi William, uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Hale Lounge, Balozi Batilda alisema tamasha hilo ni mfano wa kuigwa katika kuenzi tunu za sanaa.

“Sisi kama mkoa tumejifunza kupitia wazo hili zuri la Hale Festival. Kupitia tamasha hili, tunaweza kupata akina TX Moshi William wengi zaidi. Hongera sana Dkt. Abbas kwa maono haya,” alisema Mkuu wa Mkoa.

Katika kilele cha tamasha hilo, mwanzilishi wa Hale Festival, Dkt. Hassan Abbas, alitoa Tuzo ya Heshima (Lifetime Achievement Award) kwa marehemu TX Moshi William, kutokana na mchango wake uliotukuka katika sanaa ya muziki nchini. 

Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa familia ya marehemu, ikiwa ni alama ya shukrani na kutambua jinsi alivyounyanyua mji wa Hale na Taifa kupitia nyimbo zake zenye maadili. Alipokea mwanae marehemu, Hassan TX Moshi William Jr.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’, alimpongeza Dkt. Abbas kwa kuziunganisha bendi kongwe za Msondo Ngoma na DDC Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ jukwaa moja mjini Hale. Alisisitiza kuwa Hale Festival itumike kuandika historia ya kazi za sanaa kwa faida ya vizazi vijavyo.

“Nimefurahi kuona bendi hizi kongwe zikipiga pamoja hapa Hale. Hili la kumkumbuka TX Moshi William ni jambo zuri ambalo familia yake sasa inaona fahari kuona mzee wao anapongezwa na jamii hata baada ya kutangulia mbele za haki,”alisema MwanaFA.

Dkt. Hassan Abbas, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema msimu huu wa tatu wa tamasha hilo umeandaliwa kumuishi mwana-Hale mwenzao, Shaban Ali Muhoja Kishiwa (TX Moshi William), aliyefariki dunia Machi 24, 2006

Dkt. Abbas alikumbusha kuwa mji wa Hale ni chimbuko la magwiji wengi akiwemo Hemed Maneti, Shaban Yohana ‘Wanted’, Cosmas Chidimule, na akina Peter Kinyonga. Alibainisha kuwa TX Moshi alianzia muziki wa madebe na bendi ya ‘Songi Limata, Vumbi ya Moto’ kabla ya kuleta mageuzi makubwa kwenye muziki wa dansi.

Aidha, Dkt. Abbas alisema tamasha hilo linaambatana na mashindano ya soka ya ‘Hale Cup’ yaliyoanza Novemba 9 mwaka huu yakishirikisha vilabu 24, ambapo fainali yake inatarajiwa kupigwa Januari Mosi, 2026

Meneja wa Msondo Ngoma, Said Kibiriti, alimshukuru Dkt. Abbas kwa kumuandalia onesho hilo maalum TX Moshi, akibainisha kuwa maono yake bado ni tunu muhimu kwa jamii.

Katika tamasha hilo, muongozaji alikuwa ni mtangazaji wa ITV na Redio One Zuber Zomboko, aliwakabidhi viongozi hao, RC Batilda, MwanaFA na Dkt Abbas, frash yenye nyimbo zote alizoimba, kutunga Tx Moshi William kama sehemu ya kumuenzi gwiji hilo.

RC na MwanaFA walitoa shilingi milioni 1,500 kila mmoja kuzichangia bendi hizo kutokana na kutumbwiza na kuwaburudisha Hale na Wana Korogwe na Tanga kwa ujumla.