Dar es Salaam. Baada ya malalamiko ya wadau na wananchi kuhusu mwenendo wa ubora wa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Serikali imeagiza uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha changamoto hizo.
Kwa siku kadhaa baadhi ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wakitoa malalamiko kuhusu utendaji usioridhisha katika hospitali hiyo, yakiwamo ya kuzimwa mashine za X-ray, huku wagonjwa wakielekezwa kupata vipimo nje ya hospitali hiyo.
Wakati Serikali ikiibuka na kutoa maelekezo ya kufanyika uchunguzi, baadhi ya wadau na wananchi wameeleza malalamiko kuhusu utendaji si kwa hospitali ya Temeke pekee, bali katika maeneo mengine ya huduma za afya.
Kutokana na hayo, wameitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina kwenye maeneo yote ya utoaji huduma za afya ili kuziboresha kwa ajili ya Watanzania.
Kupitia mtandao wa jamii, mwananchi mmoja aliandika kuwa alikwenda Hospitali ya Temeke akaelezwa mashine zote za tatu za X-ray zimekufa.
“Daktari akaniambia niende kupima hospitali nyingine nije na majibu ya X-ray ili anipe majibu ya tatizo langu. Kama unabisha kesho mtu aende Hospitali ya Temeke kupima X-ray, kama atafanikiwa,” aliandika mwananchi huyo kabla ya Serikali kutoa tamko.
Mwingine Am.steveb_magari katika akaunti ya Instagram ameandika: “Hospitali nyingi za rufaa za mikoa zina rushwa zipo wazi na zinahitaji uchunguzi.”
Naye Masumbuko6047- ameandika akidai: “Kuna hospitali ya wilaya ipo Mabwepande, Kinondoni, afadhali ya Temeke utafikiri siyo hospitali ya wilaya bora ukatibiwe duka la dawa utaambuliwa hata ushauri.”
Wananchi wakitoa malalamiko hayo, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amemwelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Seif Shekalaghe kufanya uchunguzi wa kina kubaini tatizo na kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni na sheria za utumishi kwa watakaobainika kuhusika.
“Katika siku za hivi karibuni kumebainika utendaji usioridhisha katika Hospitali ya Temeke ikiwa ni pamoja na kuzimwa kwa mashine ya X-ray,” amesema Mchengerwa katika taarifa iliyotolewa kwa umma na wizara hiyo jana Desemba 26, 2025.
Taarifa hiyo imesema: “Ufuatiliaji wa siri wa Waziri Mchengerwa umebaini uwepo wa rushwa za waziwazi bila woga kuanzia kwa watumishi hadi walinzi wasio waaminifu na watoa huduma hao kwa wagonjwa. Pia wamekuwa wakiwafokea wagonjwa na kuwadhalilisha kinyume cha maadili ya kazi yao.”
Mchengerwa amewataka watumishi wa sekta ya afya kubadilika, akisema Serikali haitasita kuchukua hatua kwa watendaji wazembe, wala rushwa na wanaokiuka misingi yao maadili ya kazi.
Mbali ya hayo, Desemba 8, 2025 wakati wa kikao kazi kati yake na watumishi wa sekta ya afya kilichofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mchengerwa alikemea baadhi ya hospitali akisema kuna tuhuma za kukaa na wagonjwa kwa muda mrefu bila kutibiwa, mgonjwa kutumia miezi mingi na fedha nyingi bila kufanyiwa upasuaji.
Mchengerwa alieleza kushangazwa na Taasisi ya Mifupa MOI kukaa miezi miwili, huku mashine tatu zikiwa zimeharibika bila mategenezo. Alisema kuharibika kwa mashine hizo kumesababisha wagonjwa kukosa huduma.
“MOI mna makusanyo, viongozi mnashindwa kuidhinisha fedha mashine zikatengenezwe? Taarifa nilizonazo mashine ya Angio-Suite, CT-Scan, MRI zimeharibika miezi miwili sasa. Viongozi mpo mashine zimeharibika, wengi ni marafiki zangu lakini katika hili hapana, hii siyo staili yangu ya kufanya kazi,” alisema.
Alimwelekeza Dk Shekalaghe kufuatilia suala hilo, akisisitiza mashine yenye kazi ya upasuaji wa ubongo pasipo kufungua fuvu, lazima itengemae ili wagonjwa waendelee na matibabu.
“Nimepata pia taarifa kuna mashine hapa iliharibika kwa uzembe wa wataalamu, helium ikamwagika natoa wiki mbili nipate taarifa ya uchunguzi kuhusu hili,” alisema.
Vilevile, alizungumzia baadhi ya wagonjwa kusubiri vipimo kwa muda mrefu, akitoa mfano wa Taasisi ya Saratani Ocean Road kukaa na mashine ya Pet CT Scan kwa muda mrefu bila kuitumia.
“Mashine hii hamjaanza kutumia mnasuburi uzinduzi, wagonjwa wanakaa muda mrefu bila kupata huduma hamuwambii ukweli, mnawaingiza kwenye mchakato mwingine. Naagiza mashine hii ianze kufanya kazi si lazima waziri ndio aizindue,” alisema.
Mchengerwa alisema atapita taasisi zote zilizo chini ya wizara yake na huenda kwingine akapita usiku, ikiwemo kwenye hospitali za mikoa na kanda.
Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Katanta Simwanza, amempongeza Waziri Mchengerwa kwa hatua anazochukua akisema ni jambo la msingi kwani Watanzania wanataka kujua kitu gani kilichosababisha mashine hizo kuzimwa.
“Jambo jingine tujue changamoto hizi, zinapatikana Temeke tu au maeneo mengine? Nikiwa mtalaamu wa afya, kwenye mafunzo tunafundishwa kutoa lugha zenye staha. Hivyo ni vema tukafanya utafiti sababu zinazosababisha vikwazo katika utoaji wa huduma za afya, ikiwemo lugha na matamshi ya kutweza utu,” amesema.
Hata hivyo, Dk Simwanza amesema si watumishi pekee wanaotoa huduma za afya, bali hata wanaopewa huduma wanaotoa lugha au matamshi yasiyofaa yanayosababisha watalaamu wa sekta hiyo kuwajibu vibaya.
Amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya, ikiwamo mashine za kisasa na vifaa tiba, sambamba na uboreshaji wa vituo vya afya na hospitali.
Kwa upande wake, Waziri Kivuli wa Afya kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, Dk Elizabeth Sanga amesema taarifa ya Serikali kuhusu uchunguzi wa Hospitali ya Temeke inaonyesha ambavyo matatizo ya kitaifa ya sekta ya afya yanavyochukuliwa kama matatizo ya kipekee kwenye baadhi ya maeneo.
“Ukweli ni kwamba, kuna uharibifu wa vifaa na vitendea kazi, rushwa, huduma duni na mazingira ya hofu kwa watumishi wa afya. Hakuna uhuru wa kutoa maoni hasi. Si matatizo ya hospitali moja bali ni changamoto zilizoenea katika hospitali nyingi za umma nchini,” amesema na kuongeza:
“Kwa kulenga Temeke pekee, Serikali inaepuka kukiri na kushughulikia udhaifu wa mifumo ya ugharimiaji wa huduma za afya, usimamizi, na uwajibikaji katika sekta ya afya kwa ujumla.”
Amesema hatua hizo kuchukuliwa baada ya malalamiko ya wananchi, hilo linaonyesha kutoa matamko ya kutatua matatizo, badala ya kuyazuia kwa kuweka mifumo bora.
“Taarifa haibainishi nani ataendesha uchunguzi, kama matokeo yatawekwa wazi, au kama viongozi wa juu watawajibishwa,” amesema.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema wanasubiri uchunguzi wa kilichotokea Temeke ukamilike.
Ametoa rai kwa watumishi wa afya kote nchini kuhakikisha wanazingatia weledi.
Dk Mugisha amesema huduma za afya ni ghali, zinahitaji uwekezaji mkubwa kwenye vifaa vya kutolea huduma na matengenezo pindi vinapoharibika.
Ameeleza uwepo wa changamoto kadhaa alizosema zinaathiri utendaji.
“Vifaa tiba ni changamoto nchi nzima vikiharibika hakuna mbadala, hakuna fedha zilizotengwa kwa ukarabati, hatuna wataalamu wa kutosha wenye weledi kuvitengeneza vikiharibika,” amesema na kuongeza:
“Wengi wanatoka nje ya nchi kuja kuvitengeneza, changamoto kwenye vifaa tiba vinanunuliwa kwa mifumo ya mikataba, unakuta kikiharibika usikiguse hata kidogo, bali utoe taarifa, Serikali iunde tume ya uchunguzi kukagua kifaa ndipo kije kutengenezwa.”
Amesema ni muhimu kuimarisha mifumo yote ya kutoa huduma za afya na ikiwezekana kuwe na fedha za matengenezo, kwani hospitali zinajiendesha kwa hasara.
Mbali ya hilo, amesema inapasa kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani namna ya kutumia vifaa hivyo na kuwasomesha ili kuvifanyia matengenezo.
Anatoa mapendekezo akisema: “Serikali ifanye utafiti wa haraka na kina kubaini vyanzo vya rushwa na kutafutia suluhu ya kudumu. Pia, kutoa elimu kwa wananchi na kuwe na uwazi katika utoaji wa huduma.”
