Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ipo katika hatua za mwisho kukamilisha Sera ya Nyaraka na Kumbukumbu itakayoratibu na kusimamia masuala yote ya utunzaji wa nyaraka, ikiwa ni sehemu muhimu ya kuhifadhi na kuifahamu historia ya visiwa hivyo.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Desemba 28, 2025, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu lililopo Kilimani, Unguja, ikiwa ni katika harakati za kuadhimisha sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema Serikali imejipanga kufanya mageuzi makubwa katika Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, hususan katika utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu za Taifa.
Amesema jengo hilo lenye thamani ya zaidi ya Sh8 bilioni, litakapokamilika, litakidhi mahitaji ya sasa na ya muda mrefu kutokana na kusanifiwa kwa kuzingatia mifumo ya kiusalama, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), pamoja na mahitaji ya watumishi na wananchi wanaohitaji huduma.
Hemed amesema ili kufikia lengo la kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu kwa njia ya kidijitali, ni lazima kuwekeza katika mafunzo kwa watumishi wa taasisi hiyo ili kuwajengea uwezo wa kitaalamu unaokidhi matakwa ya kitaifa na kimataifa.
Amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na kuunga mkono juhudi zote zitakazohakikisha Zanzibar inatambulika kimataifa katika masuala ya nyaraka na kumbukumbu, ikiwa ni pamoja na kuitangaza historia ya nchi.
Amesema utunzaji sahihi wa nyaraka na kumbukumbu utachangia katika utafiti wa kitaaluma na pia kuongeza pato la Taifa kupitia sekta ya utalii, kwa kuwa kumbukumbu hizo zinaweza kuwa kivutio kwa watalii wanaotembelea Zanzibar.
Aidha, amewataka watumishi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa, akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuwafuatilia na kuwawezesha ili wafanye kazi zao kwa weledi na ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Hemed ameuagiza Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) kusimamia kwa karibu ujenzi wa jengo hilo ili mkandarasi, Kampuni ya Zeccon akamilishe kazi kwa mujibu wa mkataba unaotaka mradi huo kukamilika ndani ya miezi 18, kuanzia Machi 2024. Amesema mkandarasi atakayeshindwa kutimiza masharti ya mkataba atajinyima fursa ya kushiriki katika miradi mingine ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Dk Saada Mkuya Salum amesema Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu ni nyenzo na hazina muhimu inayoakisi maendeleo ya taifa lolote, hali iliyosababisha uamuzi wa kujenga jengo la kisasa la kuhifadhia nyaraka Zanzibar.
Dk Mkuya amesema Ofisi ya Rais Ikulu ipo katika hatua za mwisho kukamilisha Sera ya Nyaraka na Kumbukumbu itakayoboresha mfumo wa utunzaji wa nyaraka, kuangalia maslahi na vipaumbele vya watumishi, pamoja na kubadilisha taswira ya taasisi hiyo kwa kuifanya ifanye kazi kwa mifumo ya kidijitali ili kuongeza usalama wa taarifa.
“Tupo katika hatua za mwisho kukamilisha sera ya nyaraka. Kwa kutambua umuhimu wa nyaraka na kumbukumbu kwa taifa lolote, Zanzibar haina budi kuhakikisha jambo hili linapewa uzito unaostahili,” amesema Dk Saada.
Awali, akisoma taarifa ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa mradi huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Saleh Juma Mussa, amesema mradi huo hauhusishi tu kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, bali pia kuhakikisha kumbukumbu za Serikali zinahifadhiwa katika mazingira bora na salama kwa matumizi ya sasa na ya baadaye.
Amesema kwa muda mrefu Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya uhaba wa maeneo salama ya kuhifadhia nyaraka pamoja na ufinyu wa ofisi, hali iliyoisukuma Serikali kuamua kujenga jengo jipya la kisasa.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, jengo la ghorofa tano linalojengwa litagharimu zaidi ya Sh8 bilioni na litakidhi vigezo vyote vya kitaifa na kimataifa vinavyotakiwa kwa majengo ya kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu za Taifa.
“Hatua hii itatoa fursa kwa wananchi kuifahamu historia ya nchi yao kupitia kumbukumbu zitakazohifadhiwa na Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu,” amesema Saleh.