Dodoma. Watu 10 wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma baada ya kupata majeraha kwenye ajali ya basi la Super Champion, wakitoka Kilimanjaro.
Arya Mudemu, mmoja kati ya majeruhi hao amesema ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia leo Desemba 28, 2025.
Amesema walipotoka Moshi mkoani Kilimanjaro, dereva alikuwa akiendesha mwendo wa kawaida lakini baada ya kufika Babati alianza kwenda mwendo wa kasi.
Akizungumza na Mwananchi akiwa wodi namba 16 hospitalini hapo akiendelea na matibabu amesema baadhi ya abiria walipiga kelele wakimtaka dereva apunguze mwendo, lakini hakuwasikiliza.
“Kuna mahali tulipiga kelele sana lakini hatukusikilizwa,” anasema na kuongeza:
“Kwenye kona mbili zote tulikuwa tunalala upande mmoja, ndipo mbele kidogo tukajikuta tumelala chini wote. Kuna wenzetu walitoka mahututi na wengine walionekana kama wamepoteza maisha.”
Shuhuda huyo wa ajali amesema ilikuwa usiku, hivyo kuwawia ugumu wa kupata msaada.
Hata hivyo, anasema lilipita gari la familia moja lililosimama na kuwapakia majeruhi ambao walipelekwa Hospitali ya St. Gemma iliyopo Miyuji kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Dodoma, Dk Ernest Ibenzi, amekiri kupokea majeruhi 15 kutoka katika ajali hiyo.
“Ni kweli tumepokea majeruhi kutoka katika ajali hiyo. Tumewatibu, watano wameruhusiwa lakini hawa 10 bado tunao wanaendelea na matibabu ingawa hali zao zinaendelea vizuri,” amesema.
