Somalia yaikosoa Israel kuitambua Somaliland kama taifa huru

Dar es Salaam. Serikali ya Somalia imeikosoa vikali hatua ya Israel ya kuitambua rasmi Somaliland, eneo lililojitenga na Somalia kama taifa huru.

Imesema uamuzi huo ni kinyume cha sheria za kimataifa na ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya uhuru na mamlaka ya Somalia.

Kwa mujibu wa mashirika mbalimbali ya habari duniani, Somalia imeeleza hatua hiyo haina uhalali wowote wa kisheria na inalenga kudhoofisha umoja wa nchi hiyo.

Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, serikali ya Mogadishu imesisitiza haitambui uamuzi wowote wa kuitambua Somaliland kama nchi huru, ikibainisha kuwa eneo hilo bado ni sehemu ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ametangaza kuwa nchi yake itaanzisha mara moja ushirikiano wa karibu na Jamhuri ya Somaliland katika sekta za kilimo, afya, teknolojia na uchumi.

Akizungumza Ijumaa, Desemba 26, 2025, Netanyahu amesema uamuzi huo unaendana na Makubaliano ya Abraham yaliyosainiwa kwa mpango wa Rais wa Marekani, Donald Trump.

Makubaliano ya Abraham yaliyoanzishwa mwaka 2020, yalilenga kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara kati ya Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu pamoja na mataifa yenye idadi kubwa ya Waislamu.

Hata hivyo, Serikali ya Somalia imeilaani vikali hatua hiyo ya Israel, ikiitaja kuwa ni uchokozi wa makusudi dhidi ya uhuru na mamlaka ya nchi hiyo.

Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud amesema uamuzi wa Netanyahu ni kinyume na sheria na taratibu za kimataifa za kisheria na kidiplomasia.

Umoja wa Ulaya (EU) umeitaka Israel kuheshimu umoja wa Somalia, huku ukihimiza kuwepo kwa mazungumzo yenye tija kati ya Mogadishu na Somaliland ili kutatua tofauti zao kwa njia ya amani.

Somaliland iliyokuwa chini ya ulinzi wa Uingereza, ilitangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991 baada ya nchi hiyo kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Tangu wakati huo, eneo hilo limekuwa na utawala wa kujitegemea kwa kiasi kikubwa pamoja na hali ya amani na utulivu ikilinganishwa na maeneo mengine ya Somalia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeeleza inaendelea kuitambua mamlaka ya Somalia, ikijumuisha ardhi ya Somaliland.

Machi mwaka huu, Somalia na Somaliland zilikana kupokea pendekezo lolote kutoka Marekani au Israel la kuwahamisha Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza, huku Mogadishu ikisisitiza kukataa mpango wowote wa aina hiyo.

Zaidi ya nchi 20 kutoka Mashariki ya Kati na Afrika zimetangaza kupinga uamuzi wa Israel kuitambua Somaliland, zikionya kuwa hatua hiyo isiyo ya kawaida inaweza kuwa na athari kubwa kwa amani na usalama katika Pembe ya Afrika na Bahari Nyekundu.

Katika taarifa ya pamoja, iliyosainiwa pia na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), mataifa hayo yamesisitiza kukataa kuhusishwa kwa uamuzi huo na jaribio lolote la kuwafukuza kwa nguvu Wapalestina kutoka ardhi yao.

Misri imeeleza Waziri wake wa Mambo ya Nje, Badr Abdelatty, alifanya mazungumzo ya simu Ijumaa na mawaziri wenzake wa Somalia, Uturuki na Djibouti kujadili kile walichokitaja kuwa ni maendeleo hatarishi katika Pembe ya Afrika kufuatia tangazo la Israel.

Mawaziri hao walilaani uamuzi huo, wakisisitiza uungaji mkono wao kamili kwa umoja na mamlaka ya kieneo ya Somalia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeeleza kulitambua eneo lililojitenga ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa.

Kwa upande wake, Umoja wa Afrika (AU) umeukataa vikali uamuzi wowote wa kuitambua Somaliland, ukisisitiza dhamira yake isiyoyumba ya kulinda umoja na mipaka ya Somalia.

Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahmoud Ali Youssouf, amesema hatua kama hizo zinaweza kudhoofisha amani na utulivu barani Afrika.

Hadi sasa, Somaliland haijafanikiwa kupata utambuzi rasmi kutoka kwa nchi yoyote duniani. Kwa miaka kadhaa, Somalia imekuwa ikiishawishi jumuiya ya kimataifa kupinga taifa lolote linalotambua eneo hilo.

Wachambuzi wanasema kutambuliwa kwa Somaliland na Israel kunaweza kuyahamasisha mataifa mengine kufuata mkondo huo, hali itakayoongeza uzito wa kidiplomasia wa eneo hilo.