Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia na linaendelea kumuhoji Fahima Twaibu (19), msaidizi wa kazi za nyumbani kwa tuhuma za kutupa kichanga chenye jinsia ya kike, kinachokadiriwa kuwa na saa mbili tangu kuzaliwa.
Msaidizi huyo wa kazi za nyumbani mkazi wa Mtaa wa Balyehela wilayani Ilemela anadaiwa kufanya tukio hilo Desemba 25, 2025 saa 11.00 alfajiri.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatatu Desemba 29, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, mtuhumiwa Fahima Twaibu anadaiwa kutupa kichanga hicho muda mfupi baada ya kujifungua kwenye paa la nyumba inayomilikiwa na Emmanuel Muruli, ambaye ni fundi wa kuchomelea vyuma na mkazi wa Balyehela.
Mutafungwa amesema askari polisi walifika eneo hilo na kufanikiwa kuokoa maisha ya kichanga hicho kwa kushirikiana maofisa wa ustawi wa jamii pamoja na wananchi wa eneo hilo, na kukifikisha katika Hospitali ya Mkoa Sekou-Ture kwa matibabu.
”Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa ikiwemo kufikishwa mahakamani. Vitendo vya ukatili kwa watoto ni kosa la jinai na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo,” amesema Mutafungwa.
Ameongeza kusema kuwa, “tunatoa wito kwa jamii kushirikiana kwa karibu katika kulinda haki na maisha wa watoto kwa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi yao.”
Katika tukio lingine, watu wawili ambao ni wapenzi wamefariki dunia baada ya kuzuka ugomvi ambao ulisababishwa na wivu wa mapenzi.
Ambapo, Wilbert Yona (34), mfanyakazi wa kiwanda cha Ziwa Steel na mkazi wa Kata ya Ihayabuyaga, anadaiwa kumuua mpenzi wake, Marietha Kalafala (33), mfanyakazi katika Kiwanda cha Ziwa Steel na mkazi wa Mwabuyi, kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali kisha na yeye kujinyonga.
Tukio la mauaji ya Marietha Kalafala lilitokea Desemba 27, 2025 saa 2.15 usiku, katika Kitongoji cha Mwabuyi Kata ya Nyanguge wilayani Magu, aliyeuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni, mgongoni na kwenye paji la uso kisha mwili wake kutupwa kwenye shamba la mahindi.
Mutafungwa amesema baada ya ufuatiliaji ndipo Desemba 28, 2025 saa 3.00 asubuhi katika nyumba ya kulala wageni, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa mmiliki wa nyumba hiyo kuwa kuna mteja wao amejiua kwa kujinyonga kwenye chumba alichokuwa amekodi.
”Baada ya askari polisi kufika kwenye nyumba hiyo mwili wa mtu huyo ulitambuliwa kuwa ni Wilbert Yona, aliyekuwa anatafutwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Marietha Benjamini Kalafala,” amesema Mutafungwa.
Amesema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Lugeye Wilaya ya Magu, kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu na uchunguzi utakapokamilika miili hiyo itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya kuendelea na taratibu za mazishi.
”Chanzo cha matukio haya ni wivu wa mapenzi kwani inadaiwa Wilbert Yona alikuwa akimtuhumu Marietha Kalafala kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine,” amesema Mutafungwa.
Kamanda huyo ametoa wito kwa wananchi hususan wapenzi na wanandoa kuacha kujichukulia sheria mikononi wanapopata migogoro ya kimapenzi au ya kifamilia, badala yake watafute msaada wa ushauri kupitia watu wanaowaamini, ustawi wa jamii, viongozi wa dini au vituo vya huduma ya kisaikolojia.
Anaswa akitupa kichanga kwenye paa la nyumba