Unguja. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefunga kampeni zake za uchaguzi mdogo katika Jimbo la Fuoni kwa kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, ili kukipatia ushindi mkubwa na kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kampeni hizo zimehitimishwa jana Jumamosi jioni Desemba 28, 2025 katika viwanja vya Shule ya Fuoni, zikiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
Akizungumza na wananchi, Hemed amesema kazi kubwa iliyobaki ni kuhakikisha wanajitokeza mapema kumpigia kura mgombea wa CCM, Asha Hussein Saleh, huku wakilinda amani na utulivu wa nchi.
“Kazi zetu mbili zilizobaki ni kuamka mapema kwenda kupiga kura na kudumisha amani ya nchi. Tuiachie Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ifanye kazi yake,” amesema Hemed.
Amesema wananchi hawapaswi kudharau kura zao, akisisitiza kuwa kila mwenye sifa ya kupiga kura ajitokeze ili ushindi uwe mkubwa zaidi.
Hemed amesema Jimbo la Fuoni linaelekea katika hatua nzuri ya maendeleo, akitaja ujenzi wa barabara na mpango wa kujenga kituo cha afya cha kisasa, kama sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za kijamii.
Kwa upande wake, mgombea wa jimbo hilo, Asha Hussein Saleh, amesema atatekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo endapo atapewa ridhaa na wananchi, ikiwemo kuboresha huduma za maji safi na salama, umeme, elimu na huduma nyingine muhimu.
“Kwa leo sina mengi ya kusema. Naomba mjitokeze kwa wingi kukipigia kura Chama cha Mapinduzi na kunipigia mimi ili tuendelee kuleta maendeleo katika Jimbo la Fuoni,” amesema Asha.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Suzan Kunambi, amesema CCM imewaletea wananchi mgombea imara, makini na mwenye uwezo wa kuwatumikia.
“Muamini Asha akaisimamie vyema Ilani ya CCM katika Jimbo la Fuoni, kwani ana uwezo na nguvu ya kuwaletea maendeleo,” amesema Kunambi.
Ameongeza kuwa CCM kimefanya kazi kubwa ya maendeleo, hivyo wananchi wana kila sababu ya kuendelea kukiamini na kukichagua ili kifanye makubwa zaidi.
Katibu wa Oganaizesheni wa CCM Zanzibar, Ibrahim Kilupi amewataka wananchi wa Jimbo la Fuoni kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kukipatia chama hicho ushindi wa kishindo.
Kwa upande wake, Meneja wa kampeni, Hamza Hassan Chilo amesema timu ya kampeni ilipita katika kata na matawi yote ya jimbo hilo kumnadi mgombea wa CCM, huku wananchi wakiahidi kumpigia kura.
Hata hivyo, amewakumbusha wananchi kuhakikisha kila mmoja anajitokeza katika vituo vya kupigia kura siku ya uchaguzi kuchagua CCM.
Uchaguzi wa jimbo hilo utafanyika kesho Jumanne Desemba 30, 2025.