HALMASHAURI YA JIJI LA DODOMA YATOA NOTISI YA SIKU 21 KWA WADAIWA WA MALIPO YA VIWANJA MTUMBA NA KIKOMBO

……………………

Na. Meleka Kulwa- Dodoma

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetangaza orodha ya awali ya wadaiwa wa malipo ya viwanja katika maeneo ya Mtumba Zone II, Mtumba Zone III na Kikombo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa hatua za usimamizi wa ardhi ya umma.

Akizungumza na waandishi wa Habari Desemba 29,2025 Jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Dennis Harrison Gondwe, amesema kuwa wadaiwa waliotajwa katika orodha hiyo wamepewa siku 21 kuanzia tarehe 30 Desemba, 2025 ili kukamilisha malipo ya viwanja walivyopatiwa.

Amesema kuwa zoezi hilo limetokana na uhakiki wa awali uliofanywa na halmashauri kwa lengo la kuwatambua wananchi, taasisi na kampuni ambazo bado hazijakamilisha malipo ya viwanja katika maeneo husika.

Aidha, amebainisha kuwa uhakiki huo umebaini kuwepo kwa idadi kubwa ya wadaiwa ambao hawajakamilisha malipo, hali iliyoisababishia halmashauri changamoto katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ikiwemo barabara, umeme, maji na huduma nyingine muhimu.

Amesema kuwa kutokukamilika kwa malipo ya viwanja kumeathiri utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kwani fedha hizo zilipangwa kutumika katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, amesema kuwa halmashauri imeandaa na kutangaza orodha rasmi ya awali ya wadaiwa ikihusisha majina ya wadaiwa, namba za viwanja na vitalu husika, ikiwa ni hatua ya kuwakumbusha wadaiwa taarifa muhimu za viwanja vyao.

Aidha, amebainisha kuwa baada ya kumalizika kwa siku 21 za notisi, viwanja vyote ambavyo malipo yake hayajakamilika vitarudishwa sokoni kuanzia tarehe 30 Desemba, 2025.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa wito kwa wadaiwa wote wa viwanja katika maeneo ya Mtumba Zone II, Zone III na Kikombo kuhakikisha wanakamilisha malipo ndani ya muda uliowekwa.

Aidha, amebainisha kuwa mwananchi, taasisi au kampuni ambaye jina lake limo katika orodha hiyo lakini ameshakamilisha malipo anapaswa kufika katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma akiwa na nyaraka halisi za umiliki kwa ajili ya uhakiki.

Orodha ya wadaiwa inapatikana katika Gazeti la Mwananchi la tarehe 30 Desemba, 2025, tovuti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma www.dodomacc.go.tz pamoja na mitandao ya kijamii ya halmashauri kupitia Instagram @dodomacc_tz na Facebook Dodoma Council.

Kwa maelezo zaidi, wananchi wameelekezwa kufika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ofisi za iliyokuwa Manispaa ya zamani, Duka la kuuzia viwanja Namba 03, au kuwasiliana kupitia simu namba 0754 551 694 au barua pepe cd@dodomacc.go.tz.