Ibenge atumia dakika 45 kupiga chabo wapinzani

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge hajakaa kinyonge kwani baada ya mechi yao ya kwanza katika Kombe la Mapinduzi iliyopangwa kuchezwa Desemba 28, 2025 dhidi ya URA kusogezwa mbele, akaamua kuitumia siku hiyo kuwasoma wapinzani wake.

Azam iliyopangwa Kundi A katika michuano hiyo inayofanyika Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja kabla ya fainali kupigwa Gombani kisiwani Pemba, ipo na Mlandege, Singida Black Stars na URA.

Desemba 28, 2025 wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Mlandege ambayo ni bingwa mtetezi, ilifungwa mabao 3-1 na Singida Black Stars.

Katika mechi hiyo, Ibenge alitumia dakika 45 za kipindi cha kwanza kuwasoma wapinzani wake hao atakaokutana nao Desemba 31, 2025 (vs Singida) na Januari 2, 2026 (vs Mlandege).

Akiwa amekaa jukwaa kuu na wasaidizi alionao akiwamo Anicet Kiazayid, Addis Worku na Kassim Liogope, koch Ibenge alionekana kuwa makini sana kusoma mbinu za wapinzani, lakini muda alioutumia na kuondoka, akapishana na mabao kwani yote yalifungwa kipindi cha pili.

Hata hivyo, wakati Ibenge ameondoka, alimuacha Mchambuzi wa Video wa timu hiyo, Omar Boukathem ambaye alikaa hadi mwisho wa mechi na kushuhudia mbungi hiyo.

Azam ambayo ndio timu iliyotwaa mara nyingi Kombe la Mapinduzi ambazo ni tano, mbali na kucheza dhidi ya Singida Black Stars na Mlandege, itahitimisha makundi Januari 5, 2026 kwa kupambana na URA.