Jiji la Dodoma lawabana wadaiwa wa viwanja, lawapa siku 21 kulipa

Dodoma. Halmashauri ya Jiji la Dodoma imewataka wamiliki wa viwanja 6,560 vilivyoko maeneo ya Mtumba na Kikombo kulipia viwanja vyao ndani ya siku 21, ikisisitiza kuwa kushindwa kufanya hivyo kutasababisha viwanja hivyo kuhamishiwa kwa watu wengine wenye uhitaji.

Halmashauri imesema kushindwa kulipia viwanja hivyo kunakwaza utekelezaji wa bajeti yake ya utoaji wa huduma kwa wananchi, kwani fedha nyingi zimekwama katika malipo ya viwanja hivyo.

Kauli hiyo imetolewa leo, Desemba 29, 2025 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Jiji la Dodoma, Denis Gondwe, alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za jiji.

Gondwe amesema viwanja vyote 6,560 vina thamani ya Sh55.3 bilioni, na kulipwa kwa wakati kutasaidia utekelezaji wa miradi iliyopangwa kwa mwaka huu wa fedha katika bajeti ya Jiji.

“Hivi ni viwanja ambavyo wamiliki wake hawajavilipia kwa zaidi ya mwaka mmoja, wakati notisi iliwataka kufanya malipo ndani ya siku 90.

“Kuna wengine ambao wamelipia kidogo na wengine hawajalipia kabisa. Tunatoa notisi ya siku 21 ili walipie viwanja vyao, na wasipofanya hivyo watanyang’anywa na kupewa watu wengine wenye uhitaji,” amesema Gondwe.

Amesema halmashauri hiyo itawatangaza wadaiwa hao kwenye vyombo vya habari, ikiwemo gazeti la Mwananchi, ili kuwakumbusha wadaiwa waliosahau namba zao za malipo na maeneo ambayo viwanja vyao vilipo, ili wafanye malipo.

“Na kwa wale ambao watatangazwa kuwa hawajakamilisha malipo, lakini tayari wameshamaliza kulipia, wafike kwenye ofisi za jiji wakiwa na nyaraka zao za malipo ili kurekebisha kumbukumbu zao kwa usahihi,” amesema.

Gondwe amesema wadaiwa hao ni watu binafsi, taasisi na kampuni zenye viwanja katika maeneo ya Mtumba Zone 1 na 2, pamoja na eneo la Kikombo.

Amesema kucheleweshwa kwa malipo hayo kunachelewesha usambazaji wa huduma za kijamii katika maeneo hayo, ikiwemo miundombinu ya barabara, maji, umeme na huduma nyingine za msingi.‎