BAADA jana Jumapili michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 kufunguliwa kwa kuchezwa mechi moja tu kati ya Mlandege na Singida Black Stars, leo Jumatatu zinapigwa mbili ikiwamo ile ya wageni watupu wa michuano hiyo itakayofikia tamati Januari 13 mwakani.
Mapema saa 10:15 jioni, Fufuni ya Pemba itacheza dhidi ya Muembe Makumbi ya Unguja ikiwa ni mechi ya Kundi B inayohusisha wageni watupu itakayofanyika Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja.
Timu hizo zinajuana vizuri kwani zimeshakutana katika Ligi Kuu Zanzibar msimu huu na Fufuni ikaibuka na ushindi wa bao 1-0.
Katika ligi ya Zanzibar, Fufuni inaongoza msimamo ikiwa na pointi 30, wakati Muembe Makumbi ni ya nane na pointi zake 22 zote zikicheza mechi 15 zikimaliza duru la kwanza.
Kujuana kwoa huko huku Fufuni ikiwa wababe wa Muembe Makumbi, umewafanya makocha wa timu mbili kutumiana salamu mbele ya waandishi wa habari.
Kocha Mkuu wa Fufuni, Suleiman Mohammed aliesema: “Tupo tayari kuonyesha tulichonacho kama tulivyoonyesha katika Ligi ya Zanzibar. Sitaingia uwanjani na pointi zangu mfukoni, bali nitaingia na mipango ya kushinda. Ninawaheshimu Muembe Makumbi, kufa hawafi, lakini cha moto watakiona.”
Nahodha wa Fufuni, John Anthony Skwemba, amesema: “Tumejiandaa vizuri, natumaini tutafanya vizuri. Presha katika mchezo wowote haikosekani, tulichojipanga nacho ni kupata ushindi.
“Mashindano haya ni fursa kwetu kama wachezaji, tunatakiwa tutumie kadiri ya uwezo wetu ili tufanye vizuri.”
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa KVZ, Sheha Khamis amesema: “Katika Ligi tulipoteza dhidi ya Fufuni, lakini huku ni mashindano mengine, tumejipanga kushinda, kubwa zaidi nawaasa vijana wangu kuonyesha uwezo wao kupitia mashindano haya.”
Mchezaji wa KVZ, Ali Khamis Faki amesema: “Tumejipanga vizuri, Mungu akijaalia tupate matokeo mazuri na kuwapa furaha mashabiki wetu.”
Baada ya Fufuni na Muembe Makumbi kumalizana saa 10 jioni, itafuata pambano la maafande wa KVZ dhidi ya wageni wengine wa michuano hiyo, TRA United (zamani TRA).
Hii itapigwa saa 2:15 usiku ikiwa ni mechi ya Kundi C. Inazikutanisha timu moja ya Unguja na nyingine Tanzania Bara.
TRA United inashiriki kwa mara ya kwanza, huku ikipata nafasi hiyo baada ya timu kuongezwa kutoka nane za awali hadi kumi.
Kuelekea mechi hiyo, Kocha Msaidizi wa TRA United, Kassim Junior Ottieno, amesema: “Itakuwa mechi nzuri sana, timu yetu tumejiandaa vizuri, tumekuja hapa kuboresha vingi ndani ya timu. Haya mashindano kila timu ina heshima yake, kundi letu ni zuri na sio gumu wala rahisi, kwa upande wetu tumejipanga kukutana na yeyote na kushinda.
Mshambuliaji wa TRA United, Ibrahim Hamad Hilika, amesema: “Tumejipanga kufanya vizuri.”
“Makocha wetu wametuandaa vizuri wakituambia tunakwenda kuitangaza taasisi, tutahakikisha mashindano haya yatatupa kitu kizuri kuanzia mwanzo hadi mwisho kubeba ubingwa.”
Kwa upande wa KVZ, sio wageni kwani wanashiriki mara ya tatu tangu 2007 ambapo ilikuwa 2023 na 2024.
Kocha Msaidizi wa KVZ, Ali Khalid Omar, amesema: “Tunashukuru kushiriki mashindano haya ambayo sisi KVZ ni waasisi wa Kombe la Mapinduzi. Tumejiandaa kuhakikisha tunakipata tunachokihitaji.”
Bashir Muslim Daruwesh ambaye ni mchezaji wa KVZ, amesema: “Kikubwa ni kujipanga na kufuata maelekezo ya walimu, lengo kubwa ni kushinda hii mechi, tumejiandaa kufanya hivyo.”
