Mapromota, TPBRC watofautiana katiba mpya

MCHAKATO wa mabadiliko ya Katiba Mpya ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini (TPBRC) umeingia ‘mdudu’ baada ya Chama cha Mapromota wa mchezo huo (TAPBPA) kusema hakijafurahishwa na kilichofanyika na kuandika barua kulalamikia hilo nakala zikienda Baraza la Michezo (BMT) na Msajili wa Vyama na Klabu.

Mwenyekiti wa TAPBPA, Evarist ‘Mopao’ Ernest ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam akidai chama chao hakijafurahishwa na mchakato wa kuandaa katiba mpya ya TPBRC wakiamini haujawatendea haki wadau wa vyama shiriki vya mchezo huo.

Mopao amesema TPBRC liliwapa muda wa saa 24 tu kupitia rasimu ya katiba na baada ya hapo kesho yake wakatakiwa kwenda kufanya majadiliano, kitu alichodai haikuwa sawa kwani walipaswa kuisoma kwa kina na kuielewa badala ya kukurupushwa.

“Hii haikubaliki walitupa saa 24 tu yaani tupitie halafu kesho yake twende kufanya majadiliano. Tuliwaandikia barua na kuwaambia kwamba muda hautoshi wakasema hawaongezi. Mbaya zaidi hata katika kikao cha kupitia rasimu kilichofanyika kesho yake tuliambiwa twende na wajumbe wawili tu. Hii ilitunyima uhuru wa kutoa maoni yetu juu ya rasimu hiyo,” amesema Mopao mbele ya waandishi wa habari.

Kupitia taarifa ya barua pepe ambayo Mwanaspoti iliiona, TPBRC ilituma kanuni na mwaliko wa kikao kwenda TPBA Novemba 28, mwaka huu na ikakitaka chama hicho cha mapromota kufika katika kikao Novemba 29 saa 2:30 asubuhi ikiwakilishwa na wajumbe wawili.

Mwanaspoti imelitafuta Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kujua kama imepokea malalamiko yoyote kutoka kwa chama cha mapromota hao na Katibu Mkuu, Neema Msita amesema atalitolea ufafanuzi zaidi suala hilo ifikapo Januari 4 atakapokuwa amerudi katika majukumu yake rasmi baada ya kumaliza likizo.

Mwanaspoti lilipomuuliza Mopao kama TAPBPA kama imewasilisha malalamiko yoyote BMT amesema katika barua hiyo ya kuomba kuongezewa muda wa kupitia rasimu ilituma nakala pia kwenda BMT, pia wao walimtafuta Msita na kutoa malalamiko kwa njia ya mdomo na kukiri hawakuwasilisha malalamiko rasmi kwa BMT.