SEKTA YA BIMA NI MUHIMU KIUCHUMI NA KIJAMII

aziri Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware (wapili kushoto), baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo walijadiliana kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo na mustakabali wa sekta ya bima nchini pamoja na kutathmini mwenendo wa ukuaji wa sekta ya bima na mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa. Wengine katika picha ni Kamishna Msaidizi wa Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema (wa pili kulia), Naibu Kamishna wa Bima Tanzania, Bi. Khadija Issa Said (wa kwanza kulia), na Afisa Usimamizi Ubora wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Bi. Irene Horera (wa kwanza kushoto). (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)

………..

Na. Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa Sekta ya Bima ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa, hususan katika kulinda mali na shughuli za kiuchumi za wananchi na taasisi.

Mhe. Balozi Khamis amesema hayo Jijini Dar es salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ukiongozwa na Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, ambapo wamejadili masuala mbalimbali ya maendeleo na mustakabali wa sekta ya bima nchini.

Alisema kuwa Sekta hiyo ni nguzo muhimu katika ustahimilivu wa uchumi, ulinzi wa wananchi dhidi ya majanga na hatari mbalimbali, pamoja na kuchochea uwekezaji na maendeleo endelevu.

Mhe. Balozi Khamis alibainisha kuwa sekta ya bima husaidia kuongeza imani ya wawekezaji, kulinda rasilimali za Serikali na binafsi, na kupunguza mzigo wa kifedha kwa wananchi wakati wa majanga.

“Muendelee kufanya kazi nzuri kwa jamii kama Sheria ya Bima kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Bima, Sura ya 394 ilivyowapa majukumu ya kulinda haki za wadau wa bima, kutoa Elimu kwa Umma na kushughulikia malalamiko yao na Kuendeleza soko la bima kwa kuhakikisha linakuwa salama, endelevu na stahimilivu” alisema Mhe. Balozi Khamis.

Kwa upande wake Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi yake alisema kuwa, TIRA inaendelea kusimamia sekta ya Bima kwa weledi na kuifanya sekta hiyo kuendelea kukua kwa wastani wa zaidi ya asilimia 10 kwa kipindi cha miaka minne.

Dkt. Saqware alisema kuwa, Mwaka 2024 ada za bima ziliongezeka na kufikia shilingi trilioni 1.52 kutoka shilingi trilioni 1.24 mwaka 2023 ikiwa ni ongelezeko la asilimia 20.2 na mchango wa sekta ya bima kwenye pato la Taifa kuongezeka kutoka asilimia 2.01 mwaka 2023 na kufikia asilimia 2.08 mwaka 2024.

Aidha, alieleza kuwa viashiria mbalimbali vya ukuaji wa sekta ikiwemo malipo ya madai, usajili wa watoa huduma na mali na uwekezaji, ajira, na wanufaika wa bima vimeendelea kukua.

“Pamoja na mafanikio haya TIRA tumeendelea kulipa gawio kwa Serikali ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 jumla ya shilingi bilioni 5.1 zilitolewa ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo gawio lilikuwa ni shilingi bilioni 3.5 sawa na ongezeko la asilimia 68.6” aliongeza Dkt. Saqware

Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zilijadili pia changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya bima, pamoja na mikakati ya kuimarisha ushiriki wa wananchi na taasisi mbalimbali katika matumizi ya huduma za bima.

Aidha, pamoja na mambo mengine walijadiliana kuhusu masuala ya kisheria yanayoiongoza sekta hiyo, ikiwemo umuhimu wa kuendelea kufanya maboresho ya sheria na kanuni za bima ili ziendane na mabadiliko ya kiuchumi, teknolojia na mahitaji ya soko la sasa nchini.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu kamishna wa Bima Tanzania, Bi. Khadija Issa Said, Kamishna Msaidizi wa Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema, na Afisa Usimamizi Ubora wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Bi. Irene Horera.