Uchaguzi mdogo jimbo la Fuoni kesho bila ACT – Wazalendo

Unguja. Uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Fuoni, Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, unafanyika kesho, Jumanne Desemba 30, 2025, kufuatia kifo cha aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Abbas Ali Mwinyi.

Abbas Mwinyi, kaka yake mkubwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, alifariki dunia Septemba 25, 2025, alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Lumumba, Zanzibar.

Kifo hicho kilisababisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kusitisha mchakato wa uchaguzi huo uliokuwa unaendelea wakati huo.

Baada ya tukio hilo, INEC ilitangaza ratiba mpya ikijumuisha uteuzi wa wagombea, muda wa kampeni na siku ya kupiga kura, ambayo ni kesho, Jumanne Desemba 30, 2025.

Kwa mujibu wa INEC, jumla ya vyama 17 vya siasa vinashiriki uchaguzi huo. Mbali na CCM, vyama vingine ni NLD, AAFP, TLP, NRA, NCCR Mageuzi, Ada Tadea, Makini, ADC, UPDP, CCK, UMD, DP, Sau, UDP na Chaumma.

Hata hivyo, uchaguzi huo unatajwa kutokuwa na ushindani mkubwa kutokana na chama cha ACT – Wazalendo, ambacho ndicho chama kikuu cha upinzani Zanzibar, kutosimamisha mgombea katika jimbo hilo.

Kwa kawaida, siasa za Zanzibar hutawaliwa na mvuto wa vyama viwili vikuu, CCM na ACT – Wazalendo, ambavyo vina wafuasi wengi na ushawishi mkubwa miongoni mwa wananchi wa visiwa hivyo.

Awali, Mwananchi ilipokitafuta chama cha ACT – Wazalendo, kilisema kutojitokeza kwake katika uchaguzi huo kunatokana na madai ya ukiukwaji wa haki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Kwa mujibu wa chama hicho, madai hayo yaliwasukuma kufungua kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo 25. Kati ya majimbo hayo, 17 yapo Unguja na manane Pemba. Chama hicho kinadai kulikuwa na kasoro na ukiukwaji katika matokeo ya ushindi.

Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Katibu wa Itikadi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT – Wazalendo, Salim Biman, amesema kwa sasa wameelekeza nguvu kushughulikia kesi hizo mahakamani.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, CCM kilipata ushindi wa majimbo 45 ya ubunge, huku ACT – Wazalendo kikishinda majimbo matano yote yaliyopo Pemba.

Kwa upande wa uwakilishi, CCM kilishinda majimbo 40, wakati ACT – Wazalendo kilipata majimbo 10, yote yakiwa Pemba.

ACT – Wazalendo hujitambulisha kuwa na ngome yake kuu kisiwani Pemba. Uzoefu wa chaguzi zilizopita unaonesha mara nyingi chama hicho hakisimamishi wagombea katika uchaguzi mdogo unaofanyika Unguja, lakini huweka wagombea endapo uchaguzi mdogo unafanyika Pemba.

Katika baadhi ya chaguzi ndogo zilizowahi kufanyika, zikiwamo za Pandani, Konde na Mtambwe, chama hicho kiliibuka.

Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wa Jimbo la Fuoni wamesema wapo tayari kujitokeza kupiga kura licha ya maoni ya wengine kuwa uchaguzi huo hauna ushindani mkubwa.

“Kupiga kura ni haki yetu. Kwa kuwa kuna wagombea, ni muhimu kujitokeza kupiga kura ili tupate mwakilishi atakayelisimamia jimbo letu na kuleta maendeleo,” amesema mmoja wa wananchi wa jimbo hilo, Sabra Hussein.