Mbeya. Wanawake wanaojishughulisha na ufugaji wa sungura katika Kata ya Bonde la Songwe, Wilaya ya Mbeya, wameiomba Serikali na wadau kuwasaidia kupata soko la uhakika la sungura na mkojo wake ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Wamesema mkojo wa sungura, ambao umetajwa kama njia ya kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao, hususan mboga ukipatiwa soko la uhakika utawakwamua kiuchumi.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Desemba 29, 2025, mwakilishi wa kikundi hicho, Anna Simchimba, amesema mradi wa ufugaji wa sungura umekuwa mkombozi mkubwa kwao, licha ya changamoto za kukosekana kwa masoko ya uhakika.
Amesema mradi ulianza kwa ufadhili wa Shirika la Amiko, ambapo walipatiwa sungura sita, majike mawili na madume manne, ambayo sasa wamezaliana na kufikia 30.
Amesema mpaka sasa wana lita 500 za mkojo wa sungura, ambazo zimekosa wateja huku kwa mwezi wastani wa lita 20 hadi 25 zinavunwa na kuhifadhiwa.
Anna amesema kuwa wastani, kupitia kikundi chao, wanauza lita moja kati ya Sh6,000, huku maeneo mengine bei ikipanda kuanzia Sh14,000 hadi Sh15,000 kwa lita moja.
Anna amesema katika kuboresha mradi wa kufuga sungura kwa awamu ya kwanza wamepata mkopo Sh30 milioni kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
“Tumepata mkopo sasa tutapanua wigo wa ufugaji licha ya kuwepo kwa ufinyu wa eneo la kufugia kama mnavyotambua sungura wanazalisha katika eneo la wazi,” amesema.
Anna amesema licha ya kupata mkopo huo wanaiomba Serikali kutenga eneo kwa ajili ya uwekezaji wa ufugaji wa kitoweo hicho ili kupanua fursa ya ufugaji na uvunaji wa mkojo.
Akizungumza kuhusiana na soko la kitoweo hicho, Mbunge wa Mbeya vijijini, Patali Shida amewataka kuongeza tija katika ufugaji na atazungumza na Serikali kuona namna bora ili kuwakwamua kiuchumi.
Mmiliki wa Mgahawa katika Mamlaka ya Mji wa Mbalizi, Salome Noel amesema mahitaji ya sungura ni makubwa changamoto ni wao kujitangaza kupitia vipeperushi katika maeneo ya mikusanyiko ya watu.