Dar es Salaam. Mmoja wa abiria aliyesafiri kwa treni ya kisasa ya SGR kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam, na siku iliyofuata kurejea kwa usafiri huo, amesimulia adha walizokumbana nazo abiria, ikiwamo kusafiri wakiwa wamesimama, huku wengine wakilazimika kukaa sakafuni kutokana na msongamano wa abiria ndani ya treni.
Abiria huyo, Livingistoni Ruhere, kwanza alitoa simulizi hiyo kwenye ukurasa wake wa Facebook, ikiwamo picha za mnato, moja ikionesha msongamano wa abiria waliokuwa wamesimama na waliokuwa wamekaa sakafuni kwa safari yote.
Mbali na maelezo yake Ruhere kwenye ukurasa wake wa Facebook, pia alizungumza na Mwananchi akieleza kama abiria alivyopata shida kwenye safari hiyo, kwamba abiria waliokuwa na tiketi za daraja la juu (Business Class), akiwamo yeye, walilazimika kusafiri daraja la kawaida (Economy Class).
Ruhere ametoa maelezo kwenye ukurasa wake wa Facebook huku akiweka picha ya mnato ndani ya stesheni eneo la Mkonze, Dodoma, akisema: “Aibu kwa nchi yangu kituo cha SGR Mkonze hapa Dodoma leo Dec. 28. Pengine kichwa cha andiko hakipendezi, ila nadhani ndivyo hivyo.
“Abiria katika treni yetu pendwa ya SGR toka Dom kwenda Dar ya saa nane na saa 11 haikuwepo. Bahati mbaya mimi nilikuwa mmoja wa abiria wa saa 11, na nilipofika saa 10.30 tayari kwa safari, nikakuta abiria wa saa nane wamezagaa kituo hiki cha reli.
“Hii SGR ya leo 29 Desemba imenikumbusha enzi za abiria katika treni kukaa chini, kubidi kukaa vyooni. Kwanza abiria walivamia kuingia ndani na tena bila kujali daraja. Ama wengine wakalazimika kusimama, na viti vyenye nafasi ya watu wawili ikabidi waketi watatu watatu.
“Tena wenye daraja la juu, Business Class, wakasafiri madaraja ya kawaida. Nilikuwa na Business Class, bahati mbaya sijui ilivyokuwa kwa Royal Class, maana ilikuwa vigumu kufika mabehewa yake kwa kukosa namna ya kuwapita abiria waliokuwa wamesimama.”
Akizungumza na Mwananchi, Ruhere amesema kilichozua mshangao ni baadhi ya abiria waliolipia tiketi za daraja la juu (Business Class) kulazimika kusafiri wakiwa wamesimama kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, huku wengine wakiketi zaidi ya wawili kwenye kiti kimoja.
“Watu waliingia ndani ya treni kama mifugo inavyoingia zizini. Kwa umri wangu ilinibidi nitumie nguvu kujilinda. Polisi walifika kusimamia, lakini hali haikutulia na hakuna aliyekuwa anasikiliza,” amesema Ruhere.
Ameeleza kuwa uingiaji ndani ya treni ulikuwa wa msongamano mkubwa, huku watu wakivamia na kukaa kwenye viti visivyolingana na gharama za tiketi walizolipia, hali iliyosababisha ugumu wa kuwadhibiti abiria.
Ruhere amesema licha ya kukata tiketi ya Business Class, hakukuwa na utaratibu wa wazi wakati wa kupanda treni, jambo lililosababisha vurugu huku kukiwa hakuna mgawanyo kati ya abiria wa kawaida (Economy Class), wa Business wala wa VIP.
“Hakukuwa na utaratibu wowote wa wazi. Hata abiria wa VIP hawakuonekana siku hiyo,” amesema.
Ameeleza kuwa abiria wengi walifika kituoni bila kufahamu changamoto zilizokuwapo, licha ya kuwa tayari walishaarifiwa kufika kwa ajili ya safari zao.
“Hakukuwa na taarifa yoyote rasmi ya kutueleza mapema kuwa kungekuwa na changamoto. Hili ni jambo la msingi na ni haki ya abiria kupewa taarifa,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Ruhere, ucheleweshaji huo uliwakuta abiria bila kuelezwa sababu zake, licha ya uwezekano wa kuwepo kwa hitilafu za kiufundi, huku mamlaka husika zikiwa hazijatoa maelezo yoyote.
Amefafanua kuwa matukio hayo yalijirudia Desemba 28 na 29 mwaka huu, ambapo katika siku zote mbili alikuwepo katika safari hizo na hakukuwa na matangazo rasmi kwa abiria waliokwama stesheni.
Ruhere amesema Desemba 28 alitarajiwa kusafiri saa 11 alfajiri na aliwasili kituoni mapema kwa ajili ya ukaguzi, lakini baada ya kusubiri kwa muda mrefu, abiria waliarifiwa kuwa safari imeahirishwa hadi Desemba 29 saa 7 mchana bila kuelezwa sababu za mabadiliko hayo.
Mbali na picha za mnato kuhusiana na kadhia hiyo, pia kulikuwepo na picha za video jongefu zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha abiria wakiwa stesheni ya Magufuli wakilalamikia usafiri huo, huku wengine wakipaza sauti kudai kudaganywa na TRC.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Masanja, amesema abiria walionekana wamesafiri wima siyo kwamba walikosa nafasi, bali vurugu zilizozuka ndizo zilizosababisha hali hiyo.
“Tulikuwa tumepanga treni ziondoke kwa ratiba ya awali na tulitoa taarifa kwa umma, lakini ikatokea mtu mmoja alitoa taarifa isiyo ya ukweli pale pale kwamba tunawadanganya,” amesema.
Amesema ratiba ilipangwa treni kuondoka kila baada ya dakika 20, na kati ya treni hizo nne, tatu zilikuwa Dodoma, huku moja ikikaribia kushusha abiria Dar es Salaam ikikumbwa na changamoto ya kuchelewa kushusha abiria, na waliwataka abiria wasubiri kidogo.
Hata hivyo, amesema wakati maelezo hayo yakitolewa, baadhi ya wananchi walizua taharuki wakidai kuwa kulikuwa na treni moja pekee na kwamba TRC ilikuwa ikiwapotosha abiria.
Kutokana na hali hiyo, Machibya amesema tafrani ilizuka huku kila mmoja akitaka kupanda treni hiyo. Kwa kuzingatia usalama wa abiria, uongozi uliruhusu treni hiyo kuondoka mapema ili kuepusha madhara zaidi.
