DKT. KIJAJI AITAKA TFS KUHAKIKISHA DODOMA YA KIJANI

………..

Na Sixmund Begashe, Dodoma 

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji amezitaka Taasisi za Uhifadhi zilizopo chini ya Wizara kutekeleza majukumu yao kwa Weledi na kuzingatia utu ili kuakisi maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwa na Uhifadhi endelevu na kuifanya Dodoma kuwa ya Kijani. 

Wito huo umetolewa Jijini Dodoma, wakati akizungumza na Menejimenti ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) ambayo ina jukumu la kusimamia uhifadhi na kuendeleza rasilimali misitu nchini. 

Waziri Kijaji amesema kuwa, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na TFS, ni vyema ikaongeza kasi ya uhamasishaji wa upandaji miti katika Mkoa wa Dodoma ili kwenda na kasi ya Serikali chini ya Mhe. Rais Samia. 

Dkt. Kijaji amesema kuwa, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya kazi kubwa ya uhifadhi wa mazingira, hivyo jitihata hizo zinatakiwa kuungwa mkono hasa kwa kushirikisha wananchini.

Ameongeza kuwa, TFS isimamie kikamilifu suala la kupambana na uharibifu wa misitu unaotokana na uchomaji wa mkaa, ili kwenda sambamba na maono ya Rais Samia ya manutumizi ya nishati safi. 

“Mhe. Rais anapambana kuhakikisha tunaachana na nishati chafu, sasa ni wajibu wetu kuhakikisha tunasimamia ipasavyo Misitu yetu na kuepusha uchomaji wa mkaa” Alisisitiza Dkt Kijaji

Aidha Dkt. Kijaji ameongeza kuwa Mhe. Rais Samia anataka kuona urithi wa Maliasili umehifadhiwa vyema, huku nyoyo za watanzania zimegubikwa na tabasam lenye natumaini na furaha zaidi, hivyo nilazima shughuli za uhifadhi zizingatie utu wa watanzania na si vinginevyo. 

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Nkoba Mabula, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, amemuhakikishia Waziri Kijaji kuwa Ofisi yake itasimamia maelekezo yote aliyotoa kwa maslahi mapana ya Taifa. 

Katika hatua nyingine, Mhe. Kijaji, amezindia vitendea kazi vipya vya TFS ambavyo ni Magari, Ndege Nyuki na Pikipiki, huku Kamishna Mkuu wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo amesema vifaa hivyo vitatumika kikamilifu katika kuongeza ufanisi kwenye uhifadhi endelevu wa rasilimali misitu nchini.