Fufuni yaichimba mkwara Simba, kocha ajilipua

MABINGWA mara nne wa Kombe la Mapinduzi, Simba SC, imeambiwa ije kwa tahadhari kushiriki mashindano hayo kwani ratiba ya mechi zao mbili hatua ya makundi hazitakuwa rahisi.

Simba iliyopo Kundi B, imetumiwa salamu hizo na wapinzani wake, Fufuni na Muembe Makumbi City ambazo zilipokutana Desemba 29, 2025, matokeo yalikuwa 1-1.

Kocha Msaidizi wa Fufuni, Suleiman Abbas, amesema pointi moja waliyopata dhidi ya Muembe Makumbi imewapa nguvu ya wanakwenda kucheza na Simba, huku akiwaahidi mashabiki kuwapa furaha. “Simba ni timu kubwa na sisi ni wageni wa hii michuano, lakini tumekuja kushindana, hatuangalii tunacheza na nani.

“Kama tumeweka malengo ya kufika fainali na kubeba ubingwa, maana yake tunataka kuzifunga timu zote tunazokutana nazo,” amesema Abbas.

Naye Kocha Mkuu wa Muembe Makumbi City, Sheha Khamis Rashid, amesema licha ya ukubwa wa Simba, lakini wanajiandaa kuifunga na kufuzu nusu fainali.

Timu hizo zilizopo kundi B la michuano hiyo, Januari 3, 2025, Simba itacheza dhidi ya Muembe Makumbi, kisha Januari 5, 2025 ni dhidi ya Fufuni.