Dar es Salaam. Mfanyabiashara na raia wa India, Dharmendra Gaikwad (49) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kujipatia Sh457 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Gaikwad anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa madai kuwa angemuuzia Hezron Kamali, Lorry aina ya Tipa na Excavator ambayo ni mitambo inayotumika katika ujenzi, migodini na bandarini.
Mbali na Gaikwad, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ni kampuni ya Al- Zahria Tanzania Limited.
Mshtakiwa huyo amefikishwa mahakamani hapo leo Jumanne, Desemba 30, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi na wakili wa Serikali, Titus Aron.
Wakili Aron amemsomea mshtakiwa huyo mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
Hata hivyo, kabla ya kumsomea mashtaka hayo, hakimu Beda alimueleza mshtakiwa huyo kuwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.
Akimsomea mashtaka hayo, wakili Titus alidai shtaka la kwanza ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, tukio analodaiwa kulitenda Februari 28, 2025 eneo la Vingunguti, ambapo mshtakiwa alijipatia Sh82 milioni kutoka kwa Hezron Kamali, kwa madai kuwa atamununulia excavator, wakati akijua sio kweli.
Februari 14, 2025 mshtakiwa huyo alijipatia Sh40 milioni kutoka kwa Kamali kwa madai kuwa atamuuzia excavator.
Shtaka la tatu, Julai 2, 2025 eneo la Vingunguti kwa lengo la kudanganya, mshtakiwa alijipatia Sh200 milioni kutoka kwa Kamali, kwa madai kuwa atamuuzia excavator, wakati akijua sio kweli.
Tarehe hiyo pia mshtakiwa alijipatia Sh73 milioni kutoka kwa Kamali kwa madai kuwa atamuuzia Tipa, wakati akijua kuwa ni uongo.
Vile vile, mshtakiwa huyo pamoja na kampuni hiyo, walijipatia Sh62 milioni kutoka kwa mlalamikaji kwa madai kuwa wangemuuzia mtambo wa excavator.
Shtaka la sita ni kutakatisha fedha, ambapo kati ya 28 Machi na Julai 2, 2025 eneo la Vingunguti lililopo Wilaya ya Ilala, mshtakiwa alijipatia jumla ya Sh457 milioni kupitia akaunti benki ya Absa yenye jina la Al zahrin Tanzania Limited, wakati akijua ni mazalia ya kosa tangulizi la kujipatia pesa kwa udanganyifu.
Upande wa Jamhuri walidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haijakamilika hivyo wanaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Nyaki aliahirisha kesi hadi Januari 8, 2026 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
