Januari imewadia, miundombinu tayari? | Mwananchi

Dar es Salaam. Asubuhi ya Januari 13, 2026, kengele ya kwanza italia kwa mamilioni ya watoto nchini. Kwa wengine, ni mara ya kwanza kuvaa sare, kubeba mkoba mkubwa kuliko mgongo wao na kushika kalamu wakiwa na mchanganyiko wa hofu na matumaini.

Kwa wengine, ni mwanzo mpya wa safari ya sekondari hatua inayobeba ndoto na presha mpya. Lakini kabla ya sauti ya kengele hiyo, kuna swali moja kuu linalopaswa kujibiwa kwa vitendo nalo ni je, shule zetu ziko tayari?

Madarasa ni zaidi ya kuta na paa

Kwa miaka mingi, jitihada zimefanyika kujenga madarasa mapya, hasa kufuatia ongezeko la uandikishaji. Hata hivyo, Januari huja na uhalisia wake: madarasa yanakamilika bila madawati ya kutosha, au yaliyokamilika lakini hayajapokea wanafunzi kwa sababu ya upungufu wa walimu au vifaa.

Mwalimu mmoja wa shule ya msingi mkoani Morogoro anasema mara nyingi changamoto huanza siku ya kwanza ya masomo. “Unapokuta darasa lina wanafunzi zaidi ya sitini, hata ufundishaji wa kawaida unakuwa mgumu. Mtoto anayeanza darasa la kwanza anahitaji uangalizi wa karibu, si msongamano,” anaeleza.

Wanafunzi wanaoanza chekechea na darasa la kwanza wanahitaji madarasa salama, yenye mwanga, hewa na nafasi ya kucheza na kujifunza. Halikadhalika kwa wanaoanza kidato cha kwanza, msongamano darasani huathiri nidhamu, umakini na ufaulu. Serikali inapaswa kuhakikisha idadi ya madarasa inaendana na makadirio ya uandikishaji, si nadharia ya karatasini.

Vyoo na maji ni heshima na afya ya mtoto

Hakuna somo linalofundishwa kwa ufanisi pale ambapo mahitaji ya msingi hayajatimizwa. Vyoo vinavyotosheleza idadi ya wanafunzi, vilivyo salama, vinavyotenganisha jinsia na kuzingatia faragha, hasa kwa watoto wa kike ni hitaji la lazima.

Mzazi mmoja jijini Dar es Salaam Judith Mlaponi anasema uamuzi wa kumpeleka mtoto shule fulani hauzingatii matokeo pekee. “Naangalia kwanza vyoo na maji. Mtoto akikaa shule masaa mengi bila huduma hizo, hata masomo hayaingii kichwani,” anasema.

Maji safi na salama ni nguzo ya afya, usafi na heshima. Januari huleta joto na shughuli nyingi, shule zisizo na maji ya uhakika hujikuta zikiweka wanafunzi katika hatari ya magonjwa na kukosa muda wa masomo. Hapa, wajibu wa serikali ni zaidi ya kutoa maagizo; ni kuhakikisha bajeti, usimamizi na ukaguzi vinafanyika kabla ya shule kufunguliwa.

Samani na vifaa vya kukalia ili kusoma

Dawati moja kwa wanafunzi wawili si anasa, bali ni kigezo cha mazingira wezeshi. Kukaa chini au kubanana hupunguza umakini na hujenga taswira hasi ya shule kwa mtoto anayeanza safari yake ya elimu.

Afisa elimu wa halmashauri moja ya manispaa  anasema changamoto kubwa ni muda. “Fedha zinaweza kutengwa, lakini ucheleweshaji wa manunuzi husababisha samani kufika shule wakati masomo yameshaanza,” anasema, akisisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema.

Vifaa vya kufundishia vitabu, chaki na hata vifaa vya TEHAMA pale inapowezekana vinapaswa kufika shuleni kabla ya mwanafunzi, si baada ya wiki kadhaa za masomo.

Usalama na mazingira ya mwananfunzi

Shule ni makazi ya pili ya mtoto. Uzio, milango, njia salama za kuingia na kutoka, pamoja na utaratibu wa usimamizi ni muhimu. Kwa shule mpya au zilizopanuliwa, ukaguzi wa kiusalama unapaswa kufanyika kabla ya kufunguliwa.

Mtaalamu mmoja wa masuala ya elimu anaonya kuwa usalama mara nyingi husahaulika. “Tunaweza kujenga darasa zuri, lakini bila uzio au udhibiti wa mazingira yanayozunguka shule, mtoto anakuwa hatarini,” anasema.

Mazingira rafiki yanapaswa pia kuzingatia watoto wenye mahitaji maalumu, njia za kupita, vyoo na madarasa yanayozingatia ujumuishi.

Elimu ni sekta yenye wadau wengi. Wamiliki wa shule binafsi wana wajibu sawa wa kujiuliza, kwa uaminifu, kama miundombinu yao inalingana na idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa katika wiki mbili za mwanzo za Januari 2026.

Biashara ya elimu haiwezi kuachana na viwango. Madarasa yasiyotosha, vyoo vichache au ukosefu wa maji huathiri moja kwa moja ubora na usalama wa wanafunzi. Mamlaka za usimamizi zinapaswa kufanya ukaguzi wa kabla ya ufunguzi, na pale panapobidi, kusitisha uandikishaji hadi viwango vitakapofikiwa.

Aidha changamoto nyingi huanza kwenye makadirio. Serikali inapaswa kutumia takwimu za uandikishaji kwa wakati, kuoanisha na uhamaji wa watu mijini na vijijini, na kupanga rasilimali ipasavyo. Uwazi katika utoaji wa taarifa, nini kimekamilika, nini kiko njiani na wapi kuna mapungufu, hujenga imani na hushirikisha jamii katika ulinzi wa shule zao.

Wajibu wa jamii na wazazi

Ingawa wajibu wa msingi ni wa serikali na wamiliki wa shule, wazazi na jamii wana nafasi ya kuuliza maswali sahihi je, shule ina maji? Vyoo vinatosha? Mtoto wangu atakaa wapi? Maswali haya si ukaidi, bali ni ulinzi wa haki ya mtoto.

Januari 13, 2026, haitakuwa siku ya kawaida. Itakuwa kioo cha mipango yetu. Kengele italia, lakini ujumbe halisi utasikika katika ubora wa madarasa, usafi wa vyoo, mtiririko wa maji na usalama wa mazingira.

Safari ya Elimu inaanza hapa, kwa kujiuliza kama tumeandaa njia salama na stahiki kwa mtoto kuanza au kuendelea na ndoto yake. Kila jiwe la msingi likiwekwa kabla ya siku hiyo, tutakuwa tumefanya zaidi ya kufungua shule; tutakuwa tumefungua milango ya matumaini.

Alamsiki, tukutane wiki ijayo.