KIUNGO wa JKT Tanzania, Saleh Karabaka amesema japo msimu huu anataka kufunga mabao mengi ikiwezekana 20, lakini bado haamini kilichomtokea hadi sasa kwani tangu aanze kucheza Ligi Kuu ndiyo mara ya kwanza kufikisha mabao manne.
Kucheza Ligi Kuu Bara msimu wake wa kwanza ilikuwa baada ya kujiunga na Simba 2023/24 akitokea JKU ya Zanzibar, hivyo 2024/25 akiwa Namungo FC alimaliza akiwa na mabao mawili.
“Kufunga mabao manne ni rekodi mpya kwangu Ligi Kuu, lakini ninachotamani hata kufikisha mabao 20 ingawa msimu huu ni mgumu wa mapambano yanayonisaidia kujituma kwa bidii na viwango vyetu kuwa bora,” amesema Karabaka na kuongeza:
“JKT Tanzania ina malengo makubwa, hivyo kila mchezaji ana wajibu kuyapambania ili yaweze kutimia na kukabiliana na timu pinzani kupata matokeo.”
Amesema kwa nafasi ya kucheza aliyopata JKT Tanzania, anaamini msimu huu utakuwa na kitu cha tofauti kwake jina lake kutajwa miongoni mwa majina ya viungo washambuliaji wenye mabao mengi.
“Nashukuru benchi la ufundi likiongozwa na kocha mkuu Ahmad Ally anayetamani kuona kila mchezaji anafika mbali, anatujenga kuhakikisha tunautumia muda vizuri kutengeneza vitu vya tofauti katika mpira wa miguu,” amesema.
Kwa upande wake, Ally amesema: “Karabaka ni miongoni mwa wachezaji wenye uwezo mkubwa, bado ana muda mrefu wa kufanya ama kuandika rekodi iwe ndani ama nje ya Tanzania.”
