Mahakama yaamuru kesi dawa za kulevya kuanza upya

Arusha. Mahakama ya Rufaa nchini imefuta hukumu ya kifungo cha maisha jela aliyokuwa amehukumiwa Rahim Baksh Marabzay, baada ya kukiri kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini yenye uzito wa kilo 41.713 yenye thamani ya zaidi ya Sh2.085 bilioni.

Pia, mahakama hiyo imeamuru kesi hiyo irejeshwe Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa ajili ya kuanza upya hatua za kisheria kuanzia kabla ya kukabidhiwa Mahakama Kuu, huku Rahim akiendelea kukaa mahabusu kusubiri kesi hiyo kuanza upya.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa mchakato mzima wa kesi hiyo ulikuwa na dosari kubwa za kisheria, kuanzia hatua za awali za uendeshaji wa kesi.

Hukumu hiyo imetolewa Desemba 29, 2025 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa walioketi Dar es Salaam ambao ni  Ferdinand Wambali, Lucia  Kairo na Deo Nangela.

Jaji Wambali amesema Mahakama hiyo ilibaini kuwa maelezo ya mashtaka yaliyotumika kumshtaki na kumuhukumu mrufani yalikuwa na dosari kwa kumjumuisha mshtakiwa mwingine  ambaye tayari alishafariki dunia, bila kufutwa kwenye kesi kama sheria inavyotaka.

Aidha, imesema dosari hiyo ilifanya mchakato mzima wa kesi kuwa batili na kutokana na dosari hizo mrufani asingeweza kuchukuliwa kuwa alikiri kosa kwa hiari, kwani alikiri kwa kutumia maelezo  yasiyo halali kisheria.

Jaji Wambali amesema Mahakama hiyo inalazimika kupitia tena kuanzia hatua za awali za kesi hadi sababu za rufaa ambapo rekodi inaonyesha Mei 10,2017 siku ya kwanza walipofikishwa Mahakama Kuu iliahirisha kutokana na washtakiwa kuhitaji wakalimani.

Amesema rekodi inaonyesha  Mahakama Kuu ilirekodi kwamba Rasul ambaye alifariki dunia tangu  Machi 3,2017, hata hivyo, hakuna ombi la kufutwa kesi yake lililotolewa na upande wa mashtaka kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 276 (2) (kwa sasa kifungu cha 294) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai (CPA).

Zaidi ya hayo, hakuna amri inayoonyesha kwamba kesi dhidi ya marehemu ilisitishwa kama inavyohitajika na zaidi ya hayo Juni 12,2019, hakimu mwingine aliendesha kesi za kuwasilisha kesi hiyo upya na kumkabidhi mrufani na washtakiwa wengine, akiwemo marehemu kwa ajili ya kusikilizwa katika Mahakama Kuu.

Jaji amesema tatizo kuhusu kasoro hiyo halikuisha wakati wa usikilizwaji wa awali kwa sababu kesi ilipofikishwa baadaye mbele ya jaji aliyesikiliza, Septemba 9,2022, msimamo haukuwa umebadilika.

Baada ya kupitia kwa kina rekodi nzima, Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na hoja ya mrufani kuwa taarifa ya mashtaka ilitumika katika kesi hiyo ilikuwa na dosari kubwa zisizotibika, na kuwa shtaka au maelezo ya mashtaka ni msingi wa kesi ya jinai na endapo msingi huo una dosari basi mchakato mzima wa kesi unakuwa batili.

Kutokana na dosari hiyo Mahakama ilifuta hukumu ya Mahakama Kuu dhidi ya mrufani na kuamuru jalada lirejeshwe Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa ajili ya kuanza upya hatua za kisheria kabla ya kukabidhiwa Mahakama Kuu.

Kutokana na kutoridhishwa na uamuzi huo, mrufani alikata rufaa akiwa na sababu tano ikiwemo mchakato mzima wa kesi ulikuwa na dosari za kisheria, ikiwemo kumjumuisha mshtakiwa ambaye alishafariki dunia.

Nyingine ni Mahakama Kuu ilikosea kusema kuwa kukiri kwake hakukuwa na shaka, huku kukiwa hakuna marekebisho halali ya hati ya mashtaka kama inavyotakiwa na sheria.

Rahim aliyekuwa nahodha wa jahazi aina ya MV AL-Amiel iliyokuwa ikifanya safari zake Tanzania jijini Dar es Salaam, ilidaiwa Oktoba 30,2014 yeye na wenzake 12 walisafirisha dawa hizo za kulevya na kuhukumiwa Novemba 9,2022.

Ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa siku ya tukio baada ya maofisa wa Polisi kusimamisha meli hiyo mrufani huyo alikiuka amri ya polisi ambapo walianza kuwafukuza na wakati wa msako mrufani alitupa ndani ya maji kifurushi ambacho kiliaminika kuwa na dawa za kulevya.

Mrufani pamoja na Mansoor Rais, Rasul Baksh (sasa marehemu), Gulam Rezar, Nawab Bari, Said Muhamad, Nazil Pack, Mohamed Rafiq, Salim Kosal, Yari Muhamad, Allan Nuru Jawi, Razar Rais na Kheri Mohamed, walifikishwa Mahakama Kuu Dar es Salaam Mei 10,2017 baada ya shauri hilo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Januari 10,2017.

Ilidaiwa Juni 12,2019 mrufani na wenzake 11, isipokuwa Rasul (marehemu) walifikishwa Mahakama Kuu ila iliahirishwa kwa mara kadhaa hadi Novemba 9,2022 ambapo rekodi ya rufaa inaonyesha kuwa mrufani alikiri hatia huku wenzake 11 wakikana.

Hivyo mrufani alikutwa na hatia na kuhukumiwa kwa kukiuka masharti ya kifungu cha 16 (1) (b) cha Sheria ya Dawa za Kulevya, na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Rekodi inaonyesha kuwa tarehe hiyo hiyo wenzake 11 waliokana kutenda kosa hilo waliachiwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kueleza kuwa  hana nia ya kuendelea kuwashtaki washtakiwa hao.

Awali, ilidaiwa kuwa wakati wanakamatwa, kifurushi alichotupa mrufani kwenye maji kiliokotwa na polisi ambapo Oktoba 31,2014 upekuzi ulipofanyika kulikuwa Dola za Marekani 6,900 na simu ya mkononi.

Ilidaiwa cheti cha kukamatwa kiliandaliwa na kusainiwa na mrufani na shahidi huru na maofisa wa polisi, ambapo baada ya dawa hizo kuchunguzwa na mamlaka husika, ilibainika kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroini iliyokuwa na uzito wa kilo 41.713.

Mahakama Kuu ilikubali vielelezo tisa vya upande wa mashtaka ambavyo ni pamoja na hati ya upekuzi, hati ya ukamataji, ripoti ya ukaguzi wa jahazi, picha zilizochukuliwa eneo la tukio, jahazi ya MV EL-Amiel na pakiti 41 za dawa za kulevya.