MBUNGE LUTANDULA AANZA KAZI KWA KUTUMIZA AHADI YA UJENZI WA SHULE

………………

CHATO

MBUNGE wa Jimbo la Chato kusini Paschal Lutandula, ameanza kutekeleza ahadi zake kwa wananchi baada ya kukabidhi bando saba za bati kwaajili ya ukamilishaji wa jengo la utawala kwenye shule ya Sekondari Nyantimba.

Hatua hiyo inakusudiwa kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu wa takribani km 6 kutoka kijijini hapo hadi kufika ilipo shule ya Sekondari Kanyindo.

Mbali na bati hizo, amekabidhi mbao 200 za kuezekea ili kuhakikisha ifikapo Januari 2026 shule hiyo inafunguliwa na kusajili wanafunzi kuanza masomo.

Akizungumza na wananchi kwenye kijiji cha Nyantimba, Mbunge wa Jimbo hilo, amesema uamuzi huo ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa kipindi cha kampeni za Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani 2025.

“Ndugu zangu mie kwanza nimekuja kuwashukuru sana kwa kunichagua kwa kura nyingi pamoja na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, pili nimekuja kutekeleza ahadi yangu ya kuhakikisha shule yenu inakamilika na kufunguliwa kuanza kutoa elimu kwa watoto wetu”.

“Mtakumbuka wakati napita hapa kipindi cha kampeni shule hii haikuwa na hatua hii, sasa nimewaletea bati bando saba na mbao za kuezekea jengo la utawala ili mwezi wa kwanza ifunguliwe na kuanza kazi mara moja, mie siyo Mbunge wa maneno mengi bali vitendo”

“Niliahidi ndani ya siku 100 za Ubunge wangu nitatimiza ahadi hii, je nimefanya au sijafanya” amehoji wananchi.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi wenzake, mwenyekiti wa Kijiji hicho, Samwel George, amesema wapo tayali kuendelea kuzisimamia na kuzilinda raslimali zote zinazoelekezwa kwao kwa manufaa ya umma.

Amemshukuru Mbunge huyo kwa kutimiza ahadi yake na kwamba huo ndiyo uongozi wenye tija kwa jamii badala ya maneno matupu, huku akidai awali wananchi walichangishwa kiasi cha shilingi 18,000 kila kaya ili kuanzisha shule hiyo.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Elimkwasi John, amepongeza jitihada za Mbunge huyo kuisaidia serikali katika kutimiza majukumu yake kwa umma.

“Mheshimiwa Mbunge tunakupongeza sana kwa kuamua kuisiaidia serikali kutimiza wajibu wake, msaada ulioutoa ilikuwa ni jukumu la serikali lakini kwa moyo wa upendo kwa wananchi wako umeamua kutekeleza, tunakushukuru sana”.

Aidha ameahidi kuwa serikali itaendelea kusimamia kikamilifu ujenzi wa shule hiyo na kuhakikisha inasajiliwa kwaajili ya kuanza mhula wa masomo mwaka 2026.

                          Mwisho.