Msando avunja ukimya tathimini uharibifu, upotevu mali Kanisa la Gwajima

Dar es Salaam. Wakati waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima, wakisubiri msimamo wa Serikali kuhusu madai ya upotevu na uharibifu wa mali za kanisa yanayodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando amesema wamepokea tathmini hiyo na watalijibu kanisa hilo baada ya Januari Mosi, 2026.

Kanisa hilo lilifutwa usajili tangu Juni 2, 2025, kwa kile kilichoelezwa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa, kuwa limekiuka Sheria za Usajili, Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa.

Tangu usiku wa Juni 3, 2025, kanisa hilo lilikuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi, hadi Novemba 25, 2025, saa 7:30 mchana, wakati waumini waliporuhusiwa kuendelea na ibada.

Hali hiyo ilitokea siku moja baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kuagiza kanisa lifunguliwe Novemba 24, 2025.

Baada ya agizo la Waziri Mkuu na kufunguliwa kwa kanisa, uongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima ulidai kuwepo kwa upotevu na uharibifu wa mali na vifaa mbalimbali vya kanisa vyenye thamani ya Sh2.7 bilioni, hatua iliyotokea baada ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, kuagiza uongozi wa kanisa kufanya tathmini na kuwasilisha ofisini kwake kwa hatua zaidi.

Machi Mosi, 2025, kanisa liliwasilisha tathmini hiyo. Mchungaji kiongozi na Mkuu wa Utawala na Fedha wa Makanisa ya Ufufuo na Uzima, Askofu Baraka Tegge, alidai kwamba uharibifu na upotevu wa mali hizo, ikiwemo Sh420 milioni zilizokuwa kwenye shelfu maalumu, ulikuwa mkubwa.

Askofu Tegge alisema kwamba baada ya kuwasilisha tathmini hiyo, hawajapokea majibu yoyote kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya, hivyo kanisa kinasubiri ufafanuzi kabla ya kuchukua hatua zaidi kuhusiana na mali zilizoharibiwa au kupotea.

Akizungumza na Mwananchi leo, Desemba 30, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amekiri kupokea tathmini ya uharibifu na upotevu huo, na kuongeza kuwa ofisi yake itaifanyia kazi hatua hizo baada ya Januari Mosi, 2026.

“Ni kweli tumeipokea taarifa yao ya tathimini, hata hivyo tutaifanyia kazi baada ya Januari Mosi, tutaipitia kuona wameandika nini na tutawapa majibu,” amesema Msando.

Hivi karibuni uongozi wa kanisa hilo ulidai kuwasilisha tathimini hiyo tangu Desemba Mosi, bila majibu yoyote.

Askofu Tegge alipozungumza na Mwananchi alisema,”Hawajatujibu chochote baada ya kuwasilisha tathimini ya uharibifu na upotevu wa mali za kanisa.

“Tunachokisubiri ni majibu yao kuhusu uharibifu na upotevu huo, ili tujue nini tufanye, majibu yao ndiyo yatatupa mwelekeo wa jambo hili,  kama tuchukue hatua zaidi au vinginevyo.”