Mwanengo mali ya Yanga, aanza tizi la Mapinduzi

ALIYEKUWA kiungo mshambuliaji wa TRA United (zamani Tabora United), Emmanuel Mwanengo ameanza mazoezi na Yanga tayari kwa kushiriki michuano ya Mapinduzi Cup inayoendelea Zanzibar.

Mwanengo tayari ameaga TRA na kuishukuru kwa kipindi ambacho ameitumikia akiwashukuru viongozi, wachezaji na makocha aliofanyanao kazi kipindi chote akiwa na timu hiyo.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti, kuwa Mwanengo tayari wamemalizana naye, hivyo ilikuwa muhimu kuanza mazoezi na timu kwani yeye pia ni sehemu ya wachezaji wanaoenda Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 iliyoanza usiku wa juzi.

“Ndio leo (jana) amefanya mazoezi na timu kwa mara ya kwanza tangu amesajiliwa kwa mkataba wa miaka mitatu ataondoka sambamba na timu kuelekea Zanzibar kwa ajili mashindano,’  kilisema chanzo hicho na kuongeza;

MWANE 01

“Usajili unaendelea, dirisha likifunguliwa tutatambulisha wachezaji wote ambao watakuwa sehemu ya kikosi chetu hadi muda huu ni mchezaji mmoja tu ambaye ameanza mazoezi na timu.”

Mwanaspoti lilimtafuta Mwanango ili aweze kuzungumzia hilo amesema ameaga TRA kwa sababu amemaliza mkataba kuhusu kutua Yanga amesema taarifa inatolewa na uongozi yeye kazi yake ni kucheza.

“Mengi yanazungumzwa hiki ni kipindi cha usajili kama mambo yatakuwa kweli basi taarifa itatolewa na viongozi na siwezi kukataa kucheza Yanga nafasi ikitokea ni timu kubwa kila mchezaji anatamani kucheza.”

MWANE 02

Akizungumzia maisha ndani ya TRA amesema yalikuwa mazuri aliishi vizuri na wachezaji viongozi pamoja na makocha aliofanyanao kazi anawashukuru kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kuitumikia timu hiyo.

“Shukrani zote kwa watu ambao waliniamini na kunipa nafasi ya kucheza timu mbili Tabora United na sasa TRA asante nyingi kwa makocha waliokuwa sehemu ya safari yangu kisoka mwisho wa safari moja ni mwanzo wa safari nyingine, nawatakia kila la kheri.”