MATAJIRI wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC wamefungua mazungumzo na klabu ya Ghazl El Mahalla ya Misri ili kuipata saini ya beki wa kushoto wa kikosi hicho, Mtanzania Raheem Shomary kwa mkopo baada ya nyota huyo kushindwa kuwika katika Ligi ya Misri.
Nyota huyo aliyejiunga na El Mahalla, Julai 14, 2025 na kusaini mkataba wa miaka mitatu baada ya kuachana na KMC, inadaiwa hafurahii maisha ya Misri na sasa anaangalia uwezekano wa kupata timu nyingine, huku Azam ikiihitaji saini yake.
Chanzo cha karibu na mchezaji huyo, kililiambia Mwanaspoti, Shomary kwa sasa hana furaha kutokana na kutopata muda mrefu wa kucheza katika kikosi cha kwanza, jambo linalomfanya kuuomba uongozi umruhusu ili akatafute changamoto sehemu nyingine.
“Ghazl El Mahalla haikumsajili ili aende moja kwa moja katika kikosi kwa sababu malengo yao ni kuona anaendelea kupata uzoefu kwa wachezaji waliopo, ikiwa ataondoka ataruhusiwa kwenda kwa mkopo na sio vinginevyo,” kilisema chanzo hicho.
Licha ya Azam kumuhitaji katika dirisha dogo litalofunguliwa Januari 1, 2026, Haras El Hodood ya Misri pia aliyofanya majaribio kabla ya kusaini El Mahalla inahitaji saini yake hivyo, kitakachobakia ni uamuzi wake.
Kocha wa Azam, Florent Ibenge anavutiwa na beki huyo na alifanya jitihada za kumsajili kipindi akiwa na kikosi cha Al-Hilal Omdurman ya Sudan ambapo dili hilo lilikufa, japo kwa sasa anapambana tena kumnasa akiwa Azam kupitia dirisha dogo linalofunguliwa Januari 1-31 mwakani.
Raheem ni miongoni mwa nyota walioonyesha uwezo mkubwa akiwa na kikosi cha KMC, huku msimu wa 2023-2024 wa Ligi Kuu Bara, akichaguliwa mchezaji bora chipukizi, akiwashinda Semfuko Charles wa Coastal Union na Constantine Malimi wa Geita Gold.
Ubora na mwendelezo wa wachezaji hao ukafungua milango ya kuonekana na timu nyingine, ambapo Rahim akapata dili kwenda Misri, huku Semfuko Charles akajiunga na kikosi cha Simba, wakati Constantine Malimi anaitumikia Mtibwa Sugar msimu huu.
