TANZANIA YAWEKA ALAMA UWEKEZAJI AFRIKA

:::::::::

Tanzania imetajwa kushika nafasi ya tisa kati ya nchi za Afrika zenye mazingira bora ya uwekezaji kwa mwaka 2025/2026, kwa mujibu wa ripoti ya Business Insider Africa iliyorejelewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

Akizungumza jana wilayani Bagamoyo mkoani Pwani katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya uwekezaji na utoaji wa Taarifa ya Uwekezaji ya Tanzania 2025, Prof. Kitila alisema hatua hiyo inaonesha imani ya wawekezaji kwa uchumi wa nchi.

Amesema serikali imejiwekea lengo la kuhakikisha Tanzania inaingia katika orodha ya nchi tatu bora Afrika kwa kuvutia uwekezaji ifikapo mwaka 2030, kupitia maboresho ya sera na mazingira rafiki ya biashara.

Prof. Kitila alisisitiza kuwa kipaumbele cha serikali katika uwekezaji si uraia wa mwekezaji bali ni ajira zitakazozalishwa kwa Watanzania, hususan vijana, na mchango wa miradi hiyo katika kukuza uchumi.

Aidha aliwahimiza wafanyabiashara wa Kitanzania kuchangamkia fursa zilizopo, akibainisha kuwa serikali imetoa upendeleo maalum kwa wawekezaji wazawa ikiwemo ardhi bila malipo na masharti nafuu ya uwekezaji.

Kwa mujibu wa waziri huyo, serikali imeanzisha mfumo mpya wa mikataba ya uwekezaji unaowataka wawekezaji kutekeleza miradi kwa kuzingatia vigezo vya utekelezaji ili kuhakikisha ardhi na vivutio vinatoa tija kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Bw. Gilead Teri, alisema taratibu za uwekezaji kwa kampuni sita zimekamilika ndani ya Eneo Maalum la Uchumi la Bagamoyo Eco Maritime City, hatua itakayochochea ajira na uzalishaji wa viwandani.

Bw. Teri alitaja miongoni mwa miradi hiyo kuwa ni ya Canary Industries Limited, Novara Global Steel Limited na MCGA Auto Limited, ambayo kwa pamoja inatarajiwa kuwekeza mabilioni ya fedha, kutoa maelfu ya ajira na kuongeza mapato ya Serikali.